RAIS Mhe. John Magufuli amezindua rasmi Mji wa Serikali Mkoani Dodoma ambao ni Makao Makuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Jumamosi Aprili 13 ambapo amewataka watumishi wa Wizara za Serikali kuhakikisha wanaanza kutumia Ofisi hizo kuanzia Jumatatu Aprili 15.
Katika uzinduzi huo uliofanyika katika eneo la Mtumba (umbali wa kilometa 17 kutoka katikati ya Jiji la Dodoma) Rais Magufuli amewataka wakazi wa Dodoma na watanzania kwa ujumla kutumia fursa hiyo kukuza uchumi wa nchi kwa kuwekeza katika biashara mbalimbali.
“Ninawasihi Watanzania kwa ujumla kutumia fursa ya serikali kuhamia Dodoma, kama mlivyosikia zimetolewa ajira 1,288 na fursa bado zipo kama vile shule, hospitali, migahawa, kilimo na hoteli...mmeshaona Mabalozi wameshahamia hivyo tuzitumie hizi fursa kuleta maendeleo na kuijenga Dodoma ya kisasa,” alisema.
Katika hatua nyingine Mhe. Rais Magufuli amempandisha cheo aliyekuwa Luteni Kanali, Charles Mbuge kuwa Brigedia Jenerali baada ya kufurahishwa na utendaji wake wa kazi katika kusimamia ujenzi wa miradi mbalimbali ya Serikali ikiwemo ujenzi wa ukuta wa Mererani, nyumba za Serikali, nyumba za Magereza na Ofisi za Wizara kwenye Mji wa Serikali, huku akikubali ombi la kuwaajiri vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) walioshiriki katika kazi ya ujenzi kwenye operesheni kadhaa ambapo alisema idadi kubwa wataenda Jeshi la Wananchi, na wengine TAKUKURU, UHAMIAJI, POLISI, na TISS.
“Ninawapongeza maofisa walioshiriki kukamilisha mradi huu na Kanali Mbuge alisimamia ujenzi wa majengo mbalimbali ya Serikali pamoja na ukuta wa Mererani hivyo kuanzia leo nampandisha cheo atakuwa Brigedia Jerenali, sitaki kuchelewa hivyo ninataka Mkuu wa Majeshi (CDF) ukafanye utaratibu wa vile vinavyotakiwa kuwekwa kwenye mabega awekewe” alisema.
Aidha, Rais Magufuli alizipongeza taasisi mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, zilizoshiriki katika mchakato wa kufanikisha ujenzi wa Mji huo wa serikali katika eneo la Mtumba na kupongeza umoja, upendo na ushirikiano uliopo kati ya viongozi wa Wilaya na Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.