RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 11 Februari, 2021 amezindua Soko Kuu la Manispaa ya Morogoro na kuagiza soko hilo liitwe Soko Kuu la Chifu Kingalu ikiwa ni kutambua mchango wa kiongozi huyo wa kimila wa kabila la Waluguru, katika masuala mbalimbali ikiwemo utunzaji wa mazingira.
Soko hilo lenye ukubwa wa meta za mraba 9,897, vibanda vya biashara 304, vizimba 900, eneo la kuegesha magari 200 na lenye uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 2,500 limejengwa katikati ya Manisaa ya Morogoro baada ya kuvunja soko la awali lilijojengwa mwaka 1953 ambalo lilikuwa dogo na chakavu.
Ujenzi wa soko hilo umekamilika kwa asilimia 100 kwa gharama ya shilingi Bilioni 17.656 na ni miongoni mwa masoko 22 hapa nchini yaliyojengwa katika kipindi cha Serikali ya awamu ya tano kwa gharama ya shilingi Bilioni 361.033.
Baada ya kulizundua, Mhe. Rais Magufuli amewatembelea wafanyabiashara ndogondogo wanaouza bidhaa mbalimbali ndani ya soko na kusikiliza kero zao ambapo wamelalamikia kutozwa ushuru mara 2 na kwa kiwango kikubwa, na wengine kupangishwa vizimba/vibanda vya biashara na watu binafsi wakiwemo wafanyakazi wa Manispaa ya Morogoro ambao wanawatoza gharamza kubwa ikilinganishwa na gharama halisi iliyowekwa na Manispaa ya Morogoro.
Mhe. Rais Magufuli ameeleza kutofurahishwa kwake na vitengo hivyo, ameipiga marufuku Manisaa ya Mogorogoro kukusanya ushuru kwa mazao yasiyozidi tani 1 kwa mujibu wa Sheria, ameagiza wafanyakazi wa Manispaa ya Morogoro waliowapangisha vizimba/vibanda wafanyabiashara wadogo kwa kuwafanyia udalali wa kuwatoza fedha nyingi ikillinganishwa na kiwango kilichowekwa na Manispaa kurejesha fedha za juu zote kwa wahusika na kwamba kuanzia sasa wafanyabiashara waliopo kwenye vizimba/vibanda hivyo ndio watambuliwe kuwa wamiliki halali na walipe moja kwa moja Manispaa.
Amewaonya viongozi wa Mkoa wa Morogoro na taasisi zote zilizopaswa kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo na amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo kusimamia utekelezaji wa maelekezo hayo.
Mhe. Rais Magufuli amewataka Madiwani wa Manispaa ya Morogoro na Halmashauri zingine nchini kuacha mara moja kutunga Sheria ndogo zinazokinzana na Sheria mama zinazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ambavyo Manispaa ya Morogoro imetunga Sheria ndogo ya kukusanya ushuru wa mazao ya wakulima yanayoingia sokoni hapo hata kama ni kifurushi cha chini ya gunia moja ilihali Sheria inaagiza mazao yasiyozidi tani 1 yasitozwe ushuru.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameitaka Manispaa ya Morogoro kutozizuia Bodaboda na Bajaji kuingia katika Soko Kuu la Chifu Kingalu kwa kuwa vyombo hivyo ndivyo vinatumik kuweleta wananchi na bidhaa katika soko hilo na pia soko limetengewa eneo la pikipiki na bajaji.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Morogoro kwa kuongoza kitaifa katika kujitokeza kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020 ambapo asilimia 77.4 ya waliojiandikisha walipiga kura, na amewashukuru wananchi wa Mkoa huo kwa kuongoza kumpigia kura nyingi ambapo asilimia 92.3 ya waliojiandikisha walimchagua yeye wakiongozwa na Manispaa ya Morogoro iliyompa kura za Urais kwa asilimia 99.6.
Amewahakikishia kuwa atasimamia kwa nguvu zote utekelezaji wa ahadi alizozitoa na Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM (2020/25) na pia amepokea maombi ya Wabunge Mhe. Aziz Abood (Mbunge wa Morogoro Mjini) na Mhe. Innocent Kalogeris (Mbunge Morogoro Kusini) juu ya kuimarishwa kwa huduma ya maji katika Manispaa ya Morogoro, ujenzi wa barabara ya lami Kisaki – Bigwa na barabara ya Malinyi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.