RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Dodoma kutembelea miradi ya maendeleo.
Akiongea na waandishi wa habari wa Mkoa wa Dodoma ofisini kwake leo, Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Binilith Mahenge alisema kuwa ziara hiyo itaanza tarehe 21 hadi 25 Novemba, 2019.
Dkt. Mahenge alisema “natumia fursa hii kuwatangazia wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma na umma wa watanzania kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. John Pombe Magufuli, imempendeza kufanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Dodoma, makao makuu ya nchi, kuanzia tarehe 21-25 Novemba, 2019. Katika ziara hiyo atatembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Mkoa wa Dodoma na kuzungumza na wananchi”.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alizitaja shughuli zitakazofanywa na Rais kuwa, tarehe 21 Novemba, 2019 Mhe Rais atakuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 10 ya chuo kikuu cha Dodoma. Tarehe 22 Novemba, 2019 Mhe Rais atatembelea na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya hospitali ya Uhuru, wilayani Chamwino; ujenzi wa nyumba 118 za askari Polisi katika maeneo ya FFU Nzuguni na Medeli East; ujenzi wa stendi kuu ya mabasi iliyopo Nzuguni; na soko kuu linalojengwa eneo la Nzuguni. Siku hiyo itahitimishwa na mkutano wa hadhara utakaofanyika katika stendi ya mabasi Nzuguni na kurushwa moja kwa moja na vyombo mbalimbali vya habari.
Katika siku ya tatu ya ziara hiyo tarehe 25 Novemba, 2019, Mhe Rais ataweka mawe ya msingi kwenye miradi ya ujenzi wa makao makuu ya Jeshi la wananchi wa Tanzania eneo la Kikombo; ujenzi wa ofisi ya makao makuu ya idara ya Uhamiaji na ujenzi wa jengo la makandarasi katika eneo la National Capital City.
Akiongelea maandalizi ya ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa alisema kuwa maandalizi yamekamilika. “Ziara ya Mhe Rais kwetu ni fursa ya kumuonesha hatua tulizofikia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo aliyotupatia na kupokea maelekezo ya namna ya kusonga mbele kwa uhakika katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake” alisema Dkt. Mahenge.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.