Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Juni, 2020 amezindua mradi wa maji wa Kibamba - Kisarawe ambao unatekelezwa kufuatia maelekezo aliyoyatoa tarehe 21 Juni, 2017.
Sherehe za uzinduzi wa mradi huo zimefanyika Kisarawe Mkoani Pwani na kuhudhuriwa na wananchi na viongozi mbali mbali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa Dini na viongozi wa Mkoa wa Pwani wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhandisi Evarist Ndikilo.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazinginra Dar es Salaam (DAWASA) ambayo ndio imetekeleza mradi huo Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema mradi huo wenye mtandao wa Kilometa 15.65 za bomba kuu, kilometa 48 za mabomba ya usambazaji, matenki mawaili ya lita Milini 6.5 na pampu 2 umejengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 1.6 ambapo fedha zote zimetokana na makusanyo ya ndani ya DAWASA.
Mradi huo unawanufaisha wananchi wa Kata za Kisarawe, Kazimzumbani, Masali, Kibuta, Kiluvya, Kwemba, Kisopwa na Mloganzila. Pia DAWASA inapanua mradi huo kwa shilingi Bilini 7.7 ili uwafikie wananchi wa Pugu, Gongolamboto, Ukonga, Airwing, Banana, Mongolandege, Kinyerezi, Chanika na Segerea ambapo utanungana na mradi wa maji wa Ruvu Juu na Ruvu Chini.
Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa pamoja na kutekeleza agizo hilo, Wizara ya Maji imetekeleza agizo lake la kuhakikisha ukusanyaji wa mapato ya maji unaogezeka ambapo DAWASA imeongoza ukusanyaji wa mapato hayo kutoka shilingi Bilioni 2.9 kwa mwezi (mwaka 2018) hadi kukfikia shilingi Bilioni 12.3 (mwaka 2020) na kwamba kazi kama hiyo inafanyika nchi nzima ambapo miradi 192 yenye thamani ya shilingi Bilinii 163.78 inatekelezwa kwa utarativu wa 'Force Account' ambapo Serikali itaokoa zaidi ya shilingi Bilioni 48.73 ikilinganishwa na endopo itawatumia wakandarasi.
Mhe. Rais Magufuli ameipongeza DAWASA kwa utekelezaji mzuri wa mradi huo, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuwa na mpango mzuri wa upanunzi wa mtandao wa maji, hivyo ameitaka Menejimenti ya DAWASA kuboresha maslahi ya wanafanyakazi wake.
Mhe. Rais Magufuli pia ameipongeza Wizara ya Maji kwa utekelezaji wa miradi wa maji nchini ambapo katika kipindi cha miaka 5 miradi 1,423 imetekelezwa hapa nchini kwa gharama za shilingi Trilioni 3 na kwamba kutokana na juhudi hizo za Serikali hali ya upatikanaji wa maji nchini imeongezeka kutoka wastani wa asilimia 47 hadi 70.1 (Vijijini) na wastani wa silimia 74 hadi 84 (Mijini).
Katika sherehe hizo, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuanza mchakato wa ujenzi wa barabara ya lami kuunganisha Kisarawe na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na ameiagiza Wizara ya Nishati kuongeza kiwango cha umeme katika Mkoa wa Pwani ili kukidhi mahitaji yote ya kilowati 73 badala ya hali ya sasa ambapo mkoa huo unapata kilowati 30.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Kapteni Mstaafu George Mkuchika kutengua uteuzi wa Bw. Mtera Mwampamba aliyekuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Kisalawe kutokana na kashfa mbalimbali na ameagiza Bi. Mwanana Msumi ateuliwe kushika wadhifa huo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akivuta utepe pamoja na Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa ili kuzindua mradi mkubwa wa maji wa Kibamba-Kisarawe katika sherehe zilizofanyika Wilayani Kisarawe Mkoani Pwani tarehe 28 Juni, 2020.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akifungua maji kwenye eneo la mradi wa Kibamba-Kisarawe mkoani Pwani mara baada ya kuzindua mradi huo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akishika maji ya bomba mara baada ya kuzindua mradi wa maji wa Kibamba-Kisarawe.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na viongozi wengine wakifungua maji kwa pamoja kwa furaha.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.