Na. Dennis Gondwe, NALA-DODOMA
Rais wa Jamhuri ya Burundi, Meja Jenerali mstaafu Evariste Ndayishimiye amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaunganisha watanzania na warundi katika kujiletea maendeleo jijini Dodoma.
Pongezi hizo alizitoa alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa Tanzania na Burundi waliojitokeza baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha mbolea cha Intracom eneo la Nala, jijini Dodoma.
Meja Jenerali mstaafu Ndayishimiye alisema “nampongeza Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya hapa Tanzania. Rais huyu anaunganisha watanzania na warundi vizuri katika maendeleo. Anaendesha nchi vizuri na utawala bora na nchi inakwenda vizuri”.
Rais huyo wa Jamhuri ya Burundi aliishukuru Tanzania kwa kuwapokea wakimbizi kutoka Burundi. “Sasa tunaanza kuona mavuno ya huo umoja wa mababu zetu. Huwezi pumzika ukiwa tajiri kama jirani yako ni masikini, lazima umbebe mgongoni ili muende pamoja, na Tanzania imetufanyia hivyo, naona Tanzania na Burundi tunaenda pamoja” alisema Rais Meja Jenerali mstaafu Ndayishimiye.
Rais huyo aliipongeza benki ya CRDB kwa kuwekeza nchini Burundi. “Niwapongeze benki ya CRDB kwa kuja kuwekeza nchini Burundi. Tunaona CRDB inakuwa mlingoti wa fedha kutoka Tanzania kuja Burundi na kutoka Burundi kuja Tanzania, hongeza sana benki ya CRDB” alisema Meja Jenerali mstaafu Ndayishimiye.
Aidha, aliwashukuru wakazi wa Jiji la Dodoma kwa mapokezi makubwa waliyompatia. “Nawashukuru sana watu wa hapa. Tangu nimefika Dodoma mmetupokea kwa upendo sana, sasa tunajisikia kama tupo nyumbani” alisema.
Kiwanda cha mbolea cha Intracom kitakapokamilika kinasadikika kuwa kikubwa na cha aina yake katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati kikitoa ajira takribani 8,000.
Rais wa Jamhuri ya Burundi, Meja Jenerali mstaafu Evariste Ndayishimiye alipoweka jiwe la msingi la ijenzi wa kiwanda cha mbolea cha Itracom Fertilizer Limited Jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.