RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 17 Agosti, 2021 amehutubia Mkutano wa 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na kujitambulisha rasmi kwa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya hiyo.
Katika hotuba yake, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Malawi ni Taifa la kwanza katikaa nchi za SADC kuongozwa na Rais mwanamke, hivyo kujitambulisha kwake katika mkutano huo kutaongeza msukumo kwa wanawake wengi zaidi kujiamini na kuhamasisha kushiriki kwenye vyombo vya maamuzi.
Mhe. Rais Samia amewasihi viongozi wa SADC kushirikiana katika kuendeleza jitihada za kuwainua na kuwawezesha wanawake katika ngazi mbalimbali za uongozi na maamuzi katika nchi zao.
Aidha, Mhe. Rais amewafahamisha viongozi wa SADC kuwa katika mkutano wa Generation equality uliofanyika hivi karibuni nchini Ufaransa ulimchagua kuwa kinara (champion) wa masuala ya Haki za Kiuchumi za Wanawake (Women Economic Rights and Justice), hivyo kuomba ushirikiano kutoka kwao ili yeye na timu yake iweze kutekeleza jukumu hilo kikamilifu.
Amesema katika kipindi cha miaka 40 tangu kuanzishwa kwa SADC kumekuwa na mafanikio na changamoto mbalimbali, hivyo akiwa ni kiongozi mpya katika Jumuiya hiyo ameahidi kutoa ushirikiano ili kusukuma ajenda za utengano, kushughulikia changamoto na kutekeleza miango na mikakati mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumzia kuhusu kikabiliana na janga la UVIKO-19, Mhe. Rais Samia amesema lengo la Serikali yae ni kuhakikisha wananchi wote wanachanjwa ili kupata kinga ya ugonjwa huo na kuziomba Nchi za SADC kushawishi kampuni zinazozalisha chanjo kuridhia vibali na teknolojia zao zitumike ili kuruhusu chanjo kuzalishwa katika nchi mbalimbali ili kukidhi mahitaji yaliyopo.
Mhe. Rais Samia amesema ni lazima kushirikiana katika kubadilishana mbinu na uzoefu na kuwaelimisha wananchi kuhusu dhana potofu dhidi ya chanjo hizo pamoja na kuwahimiza kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na janga hilo.
Pia ameziomba Nchi zilizoendelea na Taasisi za Kifedha za Kimataifai kuendelea kutoa misamaha au kurefusha muda wa ulipaji wa madeni kwa Nchi zinazoendelea mpaka pale janga hilo litakapokwisha.
Mhe. Rais Samia amempongeza Rasi wa Malawi Dkt Lazarus Chakwera kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti mya wa SADC na ia amempongeza Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi kwa kazi kubwa na nzuri ya kuiongoza Jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Vile vile, Mhe. Rais Samia amempongeza Katibu Mtendaji wa SADC, anayemaliza muda wake Dkt. Stagomena Tax kwa kazi nzuri aliyoifanya kwenye Jumuiya hiyo kwa kipindi cha uongozi wake ambapo ameiwakilisha Tanzania katika Jumuiya hiyo.
Chanzo: Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.