Na. Dennis Gondwe, DODOMA
SERIKALI ya awamu ya sita itaendelea kulijenga Jiji la Dodoma ili liwe la kisasa na lenye hadhi ya makao makuu ya nchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi waliojitokeza katika maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa iliyofanyika kitaifa katika uwanja wa Mashujaa jijini Dodoma.
Rais Samia Suluhu Hassan alisema kuwa mwaka 2016 katika uwanja wa Mashujaa aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati Dkt. John Magufuli alitangaza dhamira ya serikali kuhamia Dodoma. Alisema kuwa serikali itaendelea kuenzi maono ya muasisi wa taifa hilo Hayati Mwalimu Julius Nyerere ya kuhamishia makao makuu ya serikali Dodoma.
Akiongelea jitihada za kulijenga Jiji la Dodoma, alisema kuwa serikali yake inaendelea na awamu ya pili ya kujenga majengo ya kudumu ya wizara katika Mji wa Serikali na yanaendelea vizuri. Alisema kuwa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Msalato unaendelea kujengwa. Alisema kuwa serikali inaendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya barabara katika jiji hilo. Jitihada nyingine alizitaja kuwa ni kupanda miti na kutunza usafi wa mazingira. “Ushujaa ni pamoja na kuiweka nchi katika uhakika wa chakula, elimu bora, umeme wa kutosha na maji” alisema Rais Samia.
Katika hatua nyingine Rais Samia alipendekeza Ofisi ya Waziri Mkuu kutafuta eneo kubwa na bora zaidi na kujenga Mnara wa Mashujaa wa makao makuu kwa gharama nafuu zinazokubalika.
Rais huyo alisisitiza wananchi kuendelea kuchanja chanjo dhidi ya UVIKO-19. Alisema kuwa kuchanja ni njia bora ya kulinda usalama wa taifa.
Vilevile, alikumbusha kuwa tarehe 23 Agosti, 2022 ni siku ya Sensa ya Watu na Makazi. Alisisitiza kila mwananchi amhimize mwenzake na kumwambia ushujaa ni kuhesabiwa.
Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 inaongozwa na kaulimbiu isemayo “Sensa kwa maendeleo, jiandae kuhesabiwa”.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama mbele ya mnara wa kumbukumbu ya mashujaa jijini Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka ngao ya jadi kwenye mnara wa mashujaa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.