RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 11 Septemba, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Bi. Amina J. Mohamed, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.
Katika mazungumzo hayo, Bi. Amina amewasilisha salamu kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na kumpongeza Mhe. Samia kwa kushika nafasi ya Urais na kumtakia heri katika majukumu yake.
Mhe. Amina amemhakikishia Mhe. Rais Samia kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kumuunga mkono katika jitihada zake mbalimbali za kuiletea Tanzania maendeleo, ikiwemo kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Aidha, amempongeza Mhe. Rais Samia kwa jitihada anazochukua dhidi ya janga la UVIKO 19 ambapo amesema Umoja wa Mataifa unaendelea kuhakikisha kuwepo kwa usawa wa upatikanaji wa chanjo na wanaendelea na majadiliano na Taasisi za Kifedha kuona namna ambavyo zinasaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na ugonjwa huo.
Vilevile, ameahidi kukunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita za kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Samia amempongeza Mhe. Amina kwa kuteuliwa tena kushika nafasi hiyo ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kumhakikishia ushirikiano zaidi kwa kuwa Umoja wa Mataifa kupitia taasisi zake mbalimbali ni mbia wa maendeleo nchini.
Mhe. Samia amemueleza Mhe. Amina kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira bora ya kibiashara na uwekezaji nchini ambapo katika kipindi cha miezi mitatu idadi ya wewekezaji imeongezeka.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (kushoto) akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bibi Amina J. Mohamed (wa pili kulia) alipofika Ikulu Chamwino kwa mazungumzo, Katikati mwenye gauni la njano ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb).
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia) na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bibi Amina J. Mohamed (kushoto) wakiwa kwenye mazungumzo Ikulu ya Chamwino, Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.