Na Eliud Rwechungura - Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameridhia kutoa kiasi cha Shilingi Bilioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 8,000 vitakavyoweza kupokea wanafunzi 400,000 kwa ajili ya ya kupokea wanafunzi Kidato cha Kwanza wanaotarajia kuanza masomo mwezi Januari, 2023 ambao ni zao la Elimumsingi bila ada.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa leo Septemba 28, 2022 jijini Dodoma Wakati akitoa maelezo kwa umma kuhusu maandalizi ya kuwapokea Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza mwakani 2023.
Bashungwa amesema fedha hizo tayari zimeingia kwenye akaunti za Shule za Sekondari 2,439 zilizoainishwa kuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa kwa ajili ya Kidato cha Kwanza 2023 na kupokelewa kwenye Halmashauri zote 184, kulingana na upungufu uliowasilishwa na kila Halmashauri husika.
Amesema pamoja na fedha za ujenzi wa madarasa mapya 8,000, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/22, ilitoa jumla ya Shilingi Bilioni 108 kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya za Kata 231 ambazo ziko katika hatua mbalimbali za ukamilishaji na zinatarajia kupokea wanafunzi mwezi Januari, 2023.
Bashungwa amefafanua kuwa kwa mwaka 2023 takribani wanafunzi 1,148,512 wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza ambapo ni wale walioanza darasa la kwanza mwaka 2016, ambapo serikali ilianza utekelezaji sera ya Elimu msingi bila ada Disemba mwaka 2015.
“Kwa mara ya kwanza, katika historia ya nchi, idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza ilikuwa kubwa sana, kwa kulinganisha na miakailiyotangulia. Kwa muktadha huo, wanafunzi waliopo Darasa la Saba mwaka 2022, ndio zao la kwanza la matokeo ya Elimumsingi Bila Ada”
Aidha, Amewaagiza Wakuu wa Mikoa nchi nzima kuhakikisha ujenzi unakamilika ndani ya miezi miwili na nusu (Siku 75 kuanzia leo) na halmashauri zitakazoshindwa kukamilisha ujenzi wa vyumba hivi vya madarasa hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya viongozi husika.
“Wakuu wa Mikoa wasimamieni Wakurugenzi kufanya matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa, na wakumbushwe kufuata Miongozo inayotolewa juu ya fedha hizo, ili kupata thamani halisi ya fedha kwa miradi inayotekelezwa” amesisitiza Bashungwa.
Wakati huo, Amewataka Wakuu wa Mikoa Kufuatilia kwa ukaribu ukamilishaji wa ujenzi wa Shule mpya kupitia mradi wa SEQUIP zikamilike kabla, au ifikapo tarehe 31 Oktoba, 2022 ili ziweze kusajiliwa na kupokea wanafunzi mwezi Januari, 2023.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.