Na. Dennis Gondwe, DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kuboresha maisha ya watanzania.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo alipokuwa akiongelea mafanikio ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa Uzinduzi wa Mikutano ya Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Waandishi wa Habari katika kampeni ya Tumekusikia Tumekufikia uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Kayombo alisema “Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika sekta ya elimu sekondari. Mheshimiwa Rais ametuletea shilingi 260,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili katika Shule ya Sekondari ya wasichana Msalato. Aidha, ameleta fedha shilingi 216,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa nane katika Shule ya Sekondari Mtemi Chiloloma. Ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa nane ya kidato cha tano na matundu 10 ya vyoo kwenye Shule ya Sekondari Zuzu”.
Akiongelea ujenzi wa shule mpya, alisema kuwa serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ili kuwaondolea kero wanafunzi ya kutembea umbali mrefu kufuata shule. “Mheshimiwa Rais ametuletea shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya nne za sekondari. Tumeletewa shilingi 544,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari Michese” alisema Kayombo.
Awali akifungua mkutano huo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema kuwa program hiyo ni muhimu kuzungumzia maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini. “Serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imekusikia imekufikia, wale wafanyakazi waliokaa miaka kadhaa mshahara haujapanda tumekusikia tumekufikia, wale waliokuwa wanateseka na maji safi na salama hayapo, tumekusikia tumekufikia, wale ambao ilikuwa ni lazima kumsafirisha mgonjwa wake kumpeleka Dar es Salaam kwenda kutibiwa tumekusikia tumekufikia, ni kampeni rahisi na inaeleka” alisema Waziri Nnauye.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.