RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema asingekuwa tayari kuhatarisha maisha yake kwa kuchanjwa chanjo ya UVIKO kama ingekuwa si salama.
Rais Samia ameyasema hayo katika uzinduzi wa uchanjaji wa chanjo, hafla iliyofanyika Ikulu Dar es Salaam, ikiwa ni baada ya wiki iliyopita taifa kuopokea zaidi ya dozi milioni 1,058,400 za chanjo zilizotolewa kupitia mpango wa upatikanaji wa chanjo Covax.
Rais amebainisha kuwa, amekubali kwa hiyari yake kuchanja akijua kwamba ndani ya mwili wake ana chanjo kadhaa ambazo ameishi nazo kwa miaka 61, kwani tangu amezaliwa kuna chanjo mbali mbali wamekuwa wakichanjwa, mbali na zingine wanazochanjwa njiani wakiwa wanasafiri ikiwemo ya homa ya manjano.
Katika mpango huo, Mhe. Rais amewaondoa hofu wananchi kuhusiana na chanjo, huku akisema yeye ni kiongozi mkuu wa nchi asingejitoa mwenyewe akajipeleka kwenye hatari huku akijua kuwa kuwa ana majukumu yanayomtegemea.
Nae, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa, afua ya chanjo inatekelezwa kote duniani na hadi kufikia tarehe 27 Julai 2021, ambapo jumla ya dozi bilini 3.9 za chanjo za UVIKO-19 zimeonesha faida nyingi zikiwemo kupunguza maambukizi, kupunguza ugonjwa mkali, kupunguza wagonjwa wanaohitaji kulazwa sababu ya UVIKO-19 na kupunguza vifo.
Aliendelea kusema kuwa, Tanzania ilifikia uamuzi wa kujiunga na mpango wa chanjo kupitia COVAX FACILITY tarehe 15 Juni, 2021 na hatimaye kupokea awamu ya kwanza ya chajo dozi 1,058,400 tarehe 24 Julai 2021.
Hata hivyo, Dkt. Gwajima amewaomba viongozi wa dini, siasa, viongozi wa kijamii katika makundi mbalimbali na watanzania wote kwa ujumla kupokea afua hii ya chanjo ambayo ndiyo silaha ya kisasa kabisa kwenye vita ya UVIKO 19 na imesaidia nchi nyingi kurudisha nyuma UVIKO 19.
Amesisitiza kuwa, Watanzania siyo wageni wa chanjo kwani miaka mingi nyuma hizi afua za chanjo zimekuwepo na mwitikio umekuwa daima mkubwa katika kutumia chanjo na kuondosha kabisa magonjwa mbalimbali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.