RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 25 Septemba, 2021 amerejea Jijini Dar es Salaam akitokea New York nchini Marekani alipokuwa akihudhuria Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhe. Rais Samia amepokelewa na Makamu wa Rais. Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla, Viongozi mbalimbali wa vyama vya Siasa, viongozi wa dini pamoja na Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Wananchi hao wamesema wamejitokeza kwa wingi kumpokea Mhe. Rais Samia na kumpongeza kutokana na kuiwakilisha vyema Tanzani kupitia hotuba yake aliyoitoa tarehe 23 Septemba, 2021 katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Mhe. Rais Samia amewashukuru wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa niaba ya Watanzania wote kwa kujitokeza kwa wingi kumpokea na kueleza kuwa htouba yake ilijikita katika mambo makuu manne.
Ameyataja mambo hayo kuwa ni kuihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kuwa Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na mataifa na wadau wengine duniani kutatua changamoto zinazoukabili ulimwengu.
Mhe. Rais Samia katika hotuba yake pia ameeleza jinsi Tanzania inavyoungana na mataifa mengine kupambana na ugonjwa wa Virus vya Korona (UVIKO), juhudi za Serikali katika kukuza uchumi na athari za mabadiliko ya Tabia Nchi.
Mhe. Rais Samia amewaomba Watanzania kuungana na kushirikiana kwa pamoja ili kuendelea kuijenga Tanzania madhubuti ambayo imejengwa kwa Zaidi ya miaka 60.
Chanzo: Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.