RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 11 Novemba, 2021 ameendelea na ziara yake ya Kiserikali katika Jamhuri ya Kiarabu ya Misri kwa kutembelea mji mpya wa Serikali wa Cairo (New Cairo Administrative City).
Serikali ya Misri ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha kuhamisha Makao Makao ya Serikali katika mji mpya. Katika mji huo mpya inatarajiwa Wizara, Taasisi za Serikali, Bunge, Mahakama, Balozi za nje zenye uwakilishi nchini Misri ikiwemo Tanzania na nyinginezo kuhamia kwenye eneo hilo ambalo pia litakapokamilika linatarajiwa kuwa na watu takribani milioni 6.5.
Aidha, Mhe. Rais Samia ametembelea eneo la viwanda la Kampuni ya Elsewedy ambao ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa nchini Misri wanaokusudia kujenga eneo la uwekezaji viwanda nchini Tanzania.
Kampuni ya Elsewedy pia ndio mkandarasi mkuu wa mradi wa Bwawa na Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere kwenye mto Rufiji.
Mhe. Rais pia ametembelea Taasisi ya uwekezaji na biashara huria (General Authority for Investment and Free Zones) ambayo ni Mamlaka Maalum iliyo chini ya Wizara ya Uwekezaji yenye dhamana ya biashara na kutoa motisha maalum kwa wawekezaji kwenye maeneo husika na pia utoaji wa vibali vya biashara na uwekezaji nchini Misri.
Katika Taasisi hiyo, Mhe. Rais Samia amekutana na wawekezaji mbalimbali na kutumia fursa hiyo kutoa wito kwa wawekezaji hao wa Misri kuja Tanzania kutumia fursa za uwekezaji zilizopo katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kilimo, madini, nishati ya umeme, elimu na nyinginezo.
Mhe. Rais Samia ameshuhudia utiaji saini wa hati za makubaliano kati ya Tanzania na Misri katika kukuza uwekezaji kwa nchi hizo mbili.
Mhe. Rais Samia akitembelea jengo jipya la makumbusho katika mji mpya wa Serikali, Cairo nchini Misri.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka saini katika kitabu cha kumbukumbu alipotembelea jengo jipya la makumbusho katika mji mpya wa Serikali, Cairo nchini Misri.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.