Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Mawaziri na Naibu Mawaziri kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na ushauri wa wataalam katika utendaji kazi pamoja na kuhuisha Sera na Sheria za nchi zilizopitwa na wakati ili ziweze kufanya kazi ipasavyo.
Mhe. Rais Samia ametoa maagizo hayo leo tarehe 13 Januari, 2022 katika Kikao Kazi na Mawaziri na Naibu Mawaziri kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Hazina, Jijini Dodoma.
Aidha, Mhe. Rais Samia amezitaka Wizara zifanye kazi kwa ushirikiano, kuwa na utaratibu pamoja na kuzingatia utunzaji wa siri za Serikali.
Mhe. Rais Samia pia amewataka Mawaziri na Naibu Mawaziri kufuatilia utendaji wa kazi wa kila Wizara kwa kutoa ripoti na takwimu sahihi na kufanya ufuatiliaji wa Miradi ili ziweze kutoa taswira sahihi ya namna ya kushugulikia na kutatua kero za wananchi.
Kwa upande mwingine, Mhe. Rais Samia amewataka viongozi hao kutenda haki na kuwa na usawa kwa watumisi walio chini yao, kufuata kanuni na miongozo ya kiserikali katika utendaji kazi na kuwachukulia hatua stahiki watumishi ambao wanabainika kukiuka kanuni na miongozo hiyo.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Samia amewaapisha Balozi Mhandisi Aisha Amour kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) na Balozi Said Shaib Mussa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kuwait.
Hafla hiyo ya uapisho imefanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.