RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassani, amewataka wanawake nchini kujiamini ili kuweza kushika nafasi za juu katika utendaji kitaifa.
Kauli hiyo ameitoa katika ukumbi wa Jakaya Kikwete wakati akizungumza na wanawake wa Jiji la Dodoma waliowawakilisha wanawake wote nchini.
Rais Hassan alisema kuwa wanawake wana mchango mkubwa kwenye shughuli za kimaendeleo, kwa kuwa wanawake hao ni jeshi kubwa kutokana na ushirikiano walionao.
“Tunatambua mchango mkubwa uliotolewa na wanawake wakati wa kulikomboa taifa letu, mavuno haya ya leo mazuri yameandaliwa na mchango wa mwanamke. Sisi tunatakiwa kuendeleza shamba hili la ukombozi” alisema Rais Hassan.
Rais huyo ameongeza kusema kuwa idadi ya viongozi wanawake imeongezeka sehemu mbalimbali ambapo katika kuwatengeneza viongozi bora wajao, ameahidi kujenga shule moja ya sekondari ya bweni kwenye kila mkoa kwa ajili ya kufundisha masomo ya sayansi kwa wasichana.
“Lengo ni kuongeza fursa ya elimu kwa upande wa wanawake wanufaike kupitia sekta ya sayansi na teknolojia. Naamini kwa kutengeneza kizazi kijacho mipango madhubuti kama hii inahitajika” alisema Rais Hassan.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima alimshukuru Rais Hassan kwa kutenga muda wake kuzungumza na wanawake kitaifa na kusema kuwa kupitia wizara yake anaahidi kutekeleza maagizo yote yatakayotolewa na rais huyo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.