RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amezindua Chuo Cha Ufundi Stadi na Huduma VETA Mkoa wa Kagera ambacho Ujenzi wake umegharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 22 ikiwa ni ufadhili kutoka Serikali ya China.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Rais Samia amemuelekeza Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo kuweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha Asilimia 10 ya Fedha za mkopo kwaajili ya Vikundi vya Vijana kinamama na Wenye ulemavu zinawanufaisha pia wahitimu wa chuo hicho kwa kuwapatia fedha taslimu au kuwanunulia Vifaa na kuwatengea maeneo ili waweze kujiajiri.
Aidha Rais Samia amesema Chuo hicho kina uwezo wa kuchukuwa wanafunzi 1,400 wa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi ambapo ameahidi kukipatia chuo Shilingi Bilioni 1 kila mwezi kwaajili ya uendeshaji ili kupunguza makali ya ada huku akijitolea kusomesha Vijana 20 ambao familia zao hazina uwezo.
Ili kuhakikisha kila Wilaya inakuwa na chuo Cha VETA, Rais Samia amesema Serikali itaendelea kutenga Shilingi Bilioni 100 Kila mwaka kwaajili ya Ujenzi wa Vyuo hivyo na kuhakikisha Wilaya zote 62 ambazo hazina chuo Cha VETA zinakuwa na chuo hicho ikiwa ni pamoja na Ujenzi wa chuo Cha VETA Mkoa wa Songwe.
Rais Samia amesema lengo Ujenzi wa Vyuo hivyo ni kuongeza thamani na ujuzi kwa vijana wanaohitimu kuanzia Elimu ya Msingi mpaka chuo wapate ujuzi wa kuwasaidia kujiajiri wenyewe ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira ambapo tafiti zinaonyesha Asilimia 12 ya Vijana hawana Ajira.
Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania, Balozi Cheng Mingjian amesema Ujenzi wa chuo hicho ni matokeo chanya ya ushirikiano baina ya Serikali ya China na Tanzania katika Mambo mbalimbali.
Chuo Cha VETA Mkoa wa Kagera kilichozinduliwa leo kina Madarasa 19 na Karakana 9 ambapo kitaanza kutoa Elimu mwezi January mwakani ambapo miongoni mwa masomo yatakayofundishwa ni Computer, ufundi wa umeme wa majumbani na viwandani, Ufundi Makenika, uchongaji vyuma, uchomeaji na uungaji vyuma, ufundi Bomba, ufundi umeme na mitambo, upakaji rangi, Ujenzi, ufundi seremala.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.