RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuimarisha usimamizi na udhibiti wa fedha za Serikali ili ziweze kutumika vizuri na kuleta tija katika miradi ya kimkakakti na kuwaletea wananchi maendeleo.
Mhe. Rais Samia amesema hayo tarehe 27 Septemba, 2021 wakati akifungua Mkutano Maalum wa Uchaguzi wa Viongozi wa ALAT uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.
Aidha, Mhe. Rais Samia ametaka kuimarishwa kwa ukusanyaji wa mapato kwa kutumia TEHAMA na kubuni vyanzo vipya vya mapato bila kutumia mabavu katika kukusanya tozo na ushuru.
Pia, Mhe. Rais Samia amewaagiza viongozi wa ALAT kuchukua hatua kwa watendaji wote watakaobainika kufanya ubadhilifu ili tija ionekane katika miradi ya maendeleo na kwenye fedha za mikopo ya asilimia 10 zinazotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Vilevile, Mhe. Rais Samia ameitaka ALAT na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwashirikisha wananchi katika kuandaa miradi ya maendeleo ya kimkakati kwani baadhi ya miradi imeshindwa kufikia malengo kutokana na ushirikishwaji mdogo ama kutoshirikishwa kwa wananchi.
Mhe. Rais Samia ametolea mfano wa baadi ya miradi kama masoko na stendi kujenga katika maeneo ambayo wananchi hawafiki na hivyo kutelekezwa au kutumika kwa kusuasua.
Aidha, Mhe. Rais Samia ameitaka Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha inapoandaa miango ya maendeleo inazingatia Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao ni wa mwisho katika kutekeleza dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025.
Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa Viongozi wa Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Kata na Vijiji kutenga siku maalum kila wiki kusikiliza na kutatua kero za wananchi zikiwemo za mirathi na migogoro ya ardhi, ambazo zimekithiri nchini.
Pia, Mhe. Rais Samia amebainisha kuwa kwa sasa kipaumbele kikubwa katika Serikali ya Awamu ya Sita ni kujenga vituo vya afya kwa Tarafa 250, upatikanaji wa maji safi na salama, ujenzi wa barabara pamoja na madarasa.
Kuhusu ujenzi wa madarasa, Mhe. Rais Samia amesema alielekeza fedha za Tozo ziende kujenga vituo vya afya na madarasa lakini sasa amepata fedha mahali ambazo zitajenga jumla ya madarasa 13,000 na kuwezesha watoto wote wanaostahili kukanza shule mwezi Januari mwaka 2022 kupata fursa hiyo.
Aidha, Mhe. Rais Samia amewataka Mameya, Wenyeviti, Madiwani na watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kushirikiana na kuacha migogoro kati yao kwa sababu tabia hiyo inazorotesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuharibu taswira ya Serikali kwa jamii.
Mhe. Rais Samia amewataka viongozi wa mikoa kuendesha kampeni ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki zoezi ya kuchanja kwa hiyari ili kujikinga na UVIKO 19, kwa kuwa ugonjwa huo bado ni tishio.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.