KATIBU TAWALA mpya wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Fatma Mganga, leo Juni 3, 2021 amepokewa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na kuanza rasmi majukumu yake huku akiahidi utumishi uliotukuka katika kuwahudumia wananchi na kutatua changamoto zinazoukabili Mkoa wa Dodoma kwenye sekta za Elimu, Uchumi, Afya, Kilimo, Mifugo na huduma nyingine za jamii kwa ujumla.
Dkt. Mganga ameyasema hayo wakati wa hafla ya kumpokea iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka wakati alipowasili kwa mara ya kwanza kama Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma kufuatia kuteuliwa kwake hivi karibuni na kuapishwa na Mheshimiwa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan Juni 2, 2021 kushika wadhifa huo.
Dkt. Mganga amesema kuwa yeye ni muumini wa kuibuka mshindi kwenye sekta zote muhimu anazozisimamia na hivyo amewataka watumishi wote wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Halmashauri za Mkoa wa Dodoma na Taasisi zote katika Mkoa huo kuwa na nidhamu, bidii na ubunifu katika kazi.
“Natambua Mkoa wa Dodoma unakabiliwa na changamoto ya Elimu na kwa muda mrefu Mkoa umekuwa na matokeo yasiyoridhisha katika mitihani ya Taifa huku ukishika nafasi ya 20 kushuka chini” Alisema Dkt. Mganga huku akiongeza kuwa ni jukumu la wanaDodoma wote kushirikiana na uongozi mpya wa Mkoa kuhakikisha hali hiyo inabadilika.
Akizigeukia Halmashauri za Mkoa wa Dodoma, Dkt. Mganga amesema kuwa anatambua changamoto zinazozikabili Halmashauri za Mkoa huo huku akiahidi kuzisimamia na kuzishughulikia akianzia na mgogoro unaoletwa na utofauti wa malipo ya waheshimiwa madiwani katika Halmashauri moja hadi nyingine za Mkoa wa Dodoma.
Aidha, ameahidi kuzisimamia kwa nguvu Halmashauri za Mkoa wa Dodoma kuhakikisha zinatenga asilimia 40% ya mapato yake na kupeleka kwenye miradi ya maendeleo na kupeleka asilimia 10% ya mapato ya ndani kwenye mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka akitoa salamu za kumkaribisha Dkt. Mganga alisema kuwa, ana imani kubwa nae na kuwa amekuwa na utendaji uliotukuka uliopelekea kupanda madaraja kutoka mtumishi wa kawaida, Mkuu wa Idara, Mkurugenzi wa Halmashauri na hadi sasa ni Katibu Tawala wa Mkoa.
“Dkt. Mganga amekuwa na rekodi nzuri ya kiutendaji wakati akiwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi na Halmashauri hiyo wakati wa kipindi chake imekuwa Halmashauri ya mfano katika Mkoa wa Dodoma na maeneo mengine ya nchi, hivyo natarajia atayaendeleza hayo yote akiwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma” aliongeza Mhe. Mtaka.
Akimuwakilisha Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma Meja Mstaafu Risasi Salingwa, amesema kuwa ili Mkoa uweze kufanikiwa na kupiga hatua lazima viongozi wa Mkoa wa Dodoma wawe na sifa za kukubali kushauri na kushauriwa, waelewe hali ya wakati uliopo na aina ya wananchi wanaowaongoza, waongoze kwa mifano na matendo bora, watumie lugha thabiti ya kiungwana, wagawe madaraka kwa wasaidizi wao na kufuatilia mrejesho wa majukumu.
Aidha, waondoe ukabila, udini na makundi ya aina zote, wazuie migongano kwa kutumia njia ya vikao na majadiliano ya mikutano na wakumbuke kuwaendeleza watumishi kwa kuwapeleka masomoni, mafunzo, kutoa motisha ya kutambua utendaji wao na pia kuwapandisha vyeo na maslahi yao, alimalizia Mwenyekiti huyo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.