Na. Theresia Francis, Dodoma
KATIBU Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Fatuma Mganga (aliyesimama pichani juu) ameongea na watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuwakumbusha sheria za utumishi wa umma, uwajibikaji, utii na nidhamu mahala pa kazi.
Dkt. Mganga amekutana na watumishi hao leo katika ukumbi wa mikutano wa jiji hilo ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya serikali katika maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma.
“Tukiitumia wiki hii ya utumishi kwa umma vizuri tutaenda kutoa huduma nzuri kwa jamii, kila mmoja kwa nafasi yake Mungu amempa baraka ya kuwa mtumishi wa umma. Sisi ndio tunabeba taswira ya mkoa katika utumishi, matamanio ya serikali ni Dodoma kuwa sehemu bora katika kutoa huduma kwa umma. Tuwe na utayari wa kusaidia likilalamikiwa jiji imelalamikiwa Dodoma tuhakikishe wananchi na wageni wanapata huduma bora,“ alisema Dkt. Mganga.
Sambamba na hilo Dkt. Mganga alieleza kuhusu madhumuni ya wiki ya utumishi kwa umma kuwa ni kuboresha ufanisi wa kazi kwa kuhakikisha kiasi cha mshahara anachopokea mtumishi wa umma kinaendana na matokeo ya kazi yake. Dhumuni lingine alilitaja kuwa ni kuwakumbusha watumishi kanuni za utumishi wa umma, kuamsha ari ya utumishi bora na utoaji huduma pamoja na kutiana moyo .
Katibu Tawala huyo aliwaasa maafisa utumishi kuwa wabunifu na kutafuta mfumo wa kubaini watumishi wanaokuwa kero kwenye utumishi wa umma na wanao haribu taswira ya utumishi. “Ninategemea kupata mrejesho namna watumishi wanafanya kazi kwa kutumia mfumo taarifa ziwe kwa mtumishi mmoja mmoja namna anavyotoa huduma, kuwahi kazini, uwajibika nakadhalika ili tuweze kutoa huduma bora” alisisitiza Dkt. Mganga.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Utawala na Rasilimali watu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Aloyce Mwogofi aliwakumbusha watumishi misingi ya utumishi kuwa ni uwajibikaji, uadilifu kazini na kusimama kwenye nafasi kama watumishi wa umma. Nyingine ni kufanya kazi kwa bidii, kujitambua na kutunza rasilimali za serikali. Vilevile, aliwakumbusha kuwa na staha ili kutoa huduma nzuri kwa wateja na kuifanya Dodoma kuwa sehemu ya mfano katika utumishi wa umma.
Mwogofi alisema “watumishi wana wajibu wa kufanya kazi kwa uadilifu, mteja akija aone amefika kwenye kimbilio la tatizo lake na anapopata huduma akiondoka ashukuru na kuwataarifu wengine kwa huduma nzuri aliyoipata. Ifike mahali mteja awe na amani na uhakika wa kupata utatuzi anapokuja ofisini kwaajili ya kupata huduma”.
Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Utawala na Rasilimali watu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Aloyce Mwogofi alipokuwa akingea na watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma leo tarehe 17 Juni, 2022 katika kuadhimisha wiki la utumishi wa umma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.