HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma leo Julai 9, 2019 imemtambulisha kocha mkuu wa timu ya soka ya ‘Dodoma Football Club’ (DFC) inayomilikiwa na Halmashauri hiyo Mbwana Makata ambapo anaanza mara moja kazi ya kuifundisha timu hiyo.
Makata ametambulishwa leo mbele ya waandishi wa habari katika ukumbi wa Jiji na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Godwin Kunambi, ambaye alisema lengo la namba la timu ya daraja la kwanza ni kupanda daraja na kucheza ligi kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2020/2021.
Kunambi alisema Halmashauri ya Jiji imeichukua timu hiyo ambayo sasa itakuwa ya wananchi kwani Halmashauri maana yake ni wananchi, huku akitoa wito kwa wakazi wote wa Dodoma kuiunga mkono ili kufikia malengo.
“Timu nyingi zinashindwa kufikia malengo kwa viongozi kuingilia kazi za makocha, kufundisha mpira ni taaluma hivyo sisi viongozi tutamkabidhi kocha kazi na kumuwezesha kila kitu ikiwemo fungu la usajili ili apate wachezaji wazuri” alisema Kunambi wakati wa Hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Meya wa Jiji hilo Mstahiki Prof. Davis Mwamfupe.
Mkurugenzi huyo alisema siri ya mafanikio katika soka ni kuwa na wachezaji wenye viwango vizuri na kufanya maandalizi kwa wakati na na kuahidi kutimiza matakwa yote ya timu kwani Halmashauri hiyo ilishatenga bajeti ya kuendesha timu hiyo katika mwaka huu mpya wa fedha.
Kwa upande wake, kocha Makata aliomba ushirikiano wa karibu kutoka kwa uongozi wa Halmashauri ya Jiji na wadau wote wa soka Jijini hapa ili kwa pamoja waweze kuivusha timu hiyo na kucheza ligi kuu mwakani.
Katika kazi hiyo mpya, Mkata atashirikiana na kocha msaidizi Renatus Shija ambaye amekuwa naye pamoja kwenye benchi la ufundi tangu walipoipandisha daraja hadi ligi kuu timu ya Allience ya Mwanza na hivi karibuni timu ya Polisi Tanzania.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.