MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge ameagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (DUWASA), na Wakala ya Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) kuhakikisha wanafikisha huduma za umeme, maji na barabara katika miradi mipya ya viwanja inayopimwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili kwenda sambasamba na mahitaji na kasi ya ujenzi unafanywa na wananchi na kuvutia zaidi wawekezaji hususan kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanja.
Ametoa maagizo hayo leo Desemba Mosi, 2020 alipofanya ziara katika maeneo mbalimbali yaliyopimwa viwanja na Jiji la Dodoma ikiwemo eneo la viwanda na eneo la taasisi za elimu ya juu yaliyopo Kata ya Nala, eneo la makazi Mahungu, Kinywambwa, Itega, Mkalama, na Iyumbu ambapo lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kukagua hali ya uendelezwaji wa maeneo hayo pamoja upatikanaji wa miundombinu muhimu hususan barabara, umeme, na maji.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru alimueleza Mkuu wa Mkoa huyo kuwa, kuchelewa kwa miundombinu hiyo ni katika baadhi ya miradi imekuwa akirudisha nyuma kasi ya uendelezaji na kwamba Jiji la Dodoma limekuwa likitoa vibali vya ujenzi kwa kasi kutokana na mahitaji makubwa ya wananchi kujenga makazi na maeneo ya biashara.
Wakuu wa taasisi za DUWASA, TARURA, na TANESCO wameelezea mipango yao mbalimbali ya haraka na ya muda mrefu katika kutoa huduma hizo muhimu katika Jiji la Dodoma ili wananchi na wawekezaji waendeleze maeneo yao kulingana na mahitaji yao.
Taasisi hizo pamoja na Halamshauri ya Jiji zimetakiwa kukutana kila mwezi ili kujadiliana kwenye maeneo yanayohitaji huduma za pamoja hususan kwenye miradi mipya ya viwanja ambavyo vinahitaji kuendelezwa kwa haraka kwa ajili ya makazi na uwekezaji mkubwa na mdogo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.