MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote katika Mkoa huo kuhakikisha wanatumia bakaa ya fedha ya mwaka wa fedha uliopita (2017/2018) pamoja na fedha za Tele-kwa-Tele kulipa madeni yote kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mkoani humo.
Alitoa maagizo hayo wakati wa kuzindua kampeni ya uhamasishaji wananchi kujiunga na mfumo wa bima ya CHF iliyoboreshwa Kimkoa iliyofanyika wilayani Mpwapwa.
Alisema agenda ya serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya kupitia mfumo wa CHF na kuziagiza Wilaya zote kufanya kampeni ya wananchi kujiunga na CHF iliyoboreshwa.
“Hakikisheni viongozi wa serikali za mtaa na vijiji wana uelewa wakutosha juu ya CHF iliyoboreshwa ili wasipokee upotoshaji juu ya mabadiliko ya gharama za uchangiaji.
Pia maofisa maendeleo ya jamii wahamasishe wananchi vya kutosha na tutashindanisha wilaya na wilaya kila baada ya miezi mitatu” alisema. Dk Mahenge pia aliagiza Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri kusimamia kwa umakini shughuli za uandikishaji ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila mwanachama wa CHF taarifa zake binafsi zimewekwa kwenye mtandao, makusanyo ya fedha yanaingizwa na yanafanywa kwa njia ya kielektroniki.
“Pia fedha za wanachama ziingizwe katika akaunti ya CHF Mkoa kwa wakati na taarifa za CHF na stakabadhi za kuwekea fedha benki ziwasilishwe kwa Katibu Tawala Mkoa mwisho wa mwezi,”alisema. Dk Mahenge aliwataka wakurugenzi hao kufuatilia utoaji huduma kwa wanachama na kama kuna changamoto wazitafutie ufumbuzi mapema ili zisiharibu taswira nzima ya mfumo wa CHF katika mkoa.
“Hii ni kazi yetu viongozi kufuatilia, ni muhimu, ...unakuta wakati mwingine hoja zinakwenda kwa viongozi wa juu kumbe zingeweza kutatuliwa katika gazi ya Kijiji au Wilaya…kasimamieni kuhakikisha CHF inakuwa agenda ya kudumu katika vikao vyote vya vijiji, au kata, wilaya hadi mkoa,” alisema.
Dkt. Mahenge aliwaagiza Wakurugenzi watendaji hao kuhakikisha kupitia bajeti za halmashauri wanatenga fedha kwa ajili ya kuhuisha kaya za wazee na kuendelea kuchangia wazee ambao hawana kadi za CHF hadi sasa na kuhakikisha vifaa kwa ajili ya huduma ya usajili wa wanachama vinanunuliwa kwa wakati.
Aliwataka Waganga wakuu wa wilaya kuhakikisha vituo vya kutolea huduma vinatumia fedha za dawa, vifaa na vifaa tiba na vitendanishi zinazoletwa kila mwezi kwa mujibu wa taratibu na miongozo iliyopo. Awali, Mbunge wa Mpwapwa, Mheshimiwa George Lubeleje alisema haipendezi kwa wanachama wa CHF kufika kwenye vituo vya afya na kutakiwa kwenda kununua dawa kutokana na vituo vya afya kukosa dawa.
Chanzo: habarileo.co.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.