Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ametoa taarifa rasmi kufanyika kwa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura mkoani Dodoma litakaloanza tarehe 25 Septemba 2024 hadi tarehe 01 Oktoba 2024.
Senyamule alisema “Dodoma inakadiriwa kuwa na wapiga kura 1,777,834 kati ya hao wamo ambao hawajawahi kujiandikisha, idadi yao hawa inakadiriwa kuwa 845,976”.
Uboreshaji huo utafanyika katika wilaya za Dodoma, Bahi, Kongwa na Chamwino. Mchakato huo utahusisha kurekebisha taarifa, uandikishaji wa wapiga kura wapya na kuwaondoa kwenye daftari waliokosa sifa, mfano waliofariki,waliofungwa kifungo cha zaidi ya miezi sita na waliopata changamoto ya afya ya akili ili kuakikisha kuwa wapiga kura wote wanaweza kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao.
Aidha, aliongeza kwa kutaja idadi ya vituo vitakavyotumika katika uboreshaji ni majengo ya Umma kama vile Ofisi za watendaji Kata, Ofisi za Watendaji wa Mitaa, Ofisi za Wenyeviti wa Vijiji, Ofisi za wenyeviti wa Vitongoji na Shule. Idadi ya vituo vya kujiandikishia Wilaya ya Dodoma ni 429, Bahi 191, Kongwa 229 na Chamwino vituo 805.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma anawasisitizia wananchi kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura wenye sifa zifuatazo; wawe wametimiza umri wa miaka 18 na kuendelea, waliojiandikisha awali na wamehama kata au jimbo, wenye taarifa zilizokosewa wakati wa uandikishaji na waliopoteza au kadi zao kuharibika.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.