SERIKALI ya Mkoa wa Dodoma imewataka wafanyabiashara wadogo wote kuwa na vitambulisho vya wajasiriamali vilivyotolewa na Mhe. Rais ili waweze kufanya biashara zao bila usumbufu wowote.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge alipokuwa akiongea na wafanyabiashara wadogo katika soko la Bonanza lililopo Kata ya Chamwino jana.
Dkt. Mahenge alisema kuwa, dhamira ya Rais Mhe. Dkt. John Magufuli ni kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kufanya biashara zao pasipokuwa na usumbufu wa tozo mbalimbali.
“Maelekezo yangu ni kwamba kuanzia kesho Mei 22, 2019 muwe na vitambulisho vya wajasiriamali vilivyotolewa na Mhe. Rais kwa faida yenu…kigezo cha kuwa na kitambulisho ni mtaji wako, siyo meza unayofanyia biashara, mtaji ndiyo unaokutambulisha kuwa wewe ni wa kitambusho cha shilingi 20,000 au wewe ni wa Mamlaka ya Mapato Tanzania…haitaruhusiwa mtu kufanya biashara bila kitambulisho na ukivaa kitambulisho hakuna mtu kukudai ushuru” alisisitiza Dkt. Mahenge.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa, kwa wafanyabiashara ambao mtaji wao unazidi shilingi milioni nne, wao wanatakiwa kusajiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania ili kulipa kodi ya Serikali.
“Kwa wafanyabiashara ambao mtaji wao hauzidi shilingi milioni nne, Mheshimiwa Rais amesema mtalipa shilingi 20,000 kwa mwaka mzima na kupewa kitambulisho” alisisitiza Dkt. Mahenge.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara wadogo kufuata taratibu na sheria zilizopo katika kutekeleza majukumu yao ikiwemo kufanya usafi katika masoko, na kuepuka kupanga biashara zao kwenye maeneo yasiyoruhusiwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alisema “maekelezo ya Mkuu wa Mkoa ni maelekezo halali…lengo la Mheshimiwa Rais ni kuwatumikia wananchi wanyonge ili wakuze mitaji yao na kuwa wafanyabiashara wakubwa” alisema Kunambi.
Alisema Halmashauri inatakiwa kufikiri tofauti, kuwa na mapato ya ndani ya kudumu.
“Haiingii akilini kufikiri kwamba Halmashauri ya Jiji kama letu itegemee ‘petty collection’ kujiendesha” aliongeza Kunambi.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alitembelea masoko ya Bonanza-Chamwino na Chang’ombe kuongea na wafanyabiashara wadogo akiambatana na Katibu Tawala Mkoa Maduka Kessy, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa na Wilaya.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.