MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge amezitaka halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya kupokea wawekezaji ili kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza katika Mkoa wa Dodoma hasa baada ya kuwa makao makuu na kuwa na fursa nyingi.
Dkt Mahenge ametoa maagizo hayo jijini Dodoma wakati wa kikao cha kamati ya ushauri cha Mkoa (RCC) ambapo amesema bado kuna changamoto katika maandalizi katika halmashauri nyingi pindi zinapopokea wawekezaji.
Amezitaka halmashauri zote kuweka mazingira mazuri hasa katika kuwapokea wawekezaji na namna ya kuwahendo wawekezaji pindi wanapoingia katika maeneo yao kwa lengo la kutaka kuwekeza maeneo hayo.
“Nataka maeneo yote yawe tayari kwa ajili ya uwekezaji muwekezaji anapokuja anataka huduma zote za muhimu ziwepo katika eneo husika, sio muwekezaji anakuja unaambiwa ukianza ujenzi ndio tunakuletea huduma za maji, umeme na barabara” amesema Dkt Mahenge.
Aidha amewataka viongozi wa ngazi zote katika halmashauri kuweka mkazo katika kusimamia miradi ya maendeleo hasa miradi ya maji ambapo tatizo limekuwa sugu katika maeneo mbalimbali kwa usimamizi hafifu kutoka kwa viongozi.
“Katika maeneo mengi miradi hasa ya maji haikamiliki kwa wakati, hii sio miradi ya RUWASA peke yao hii ni miradi ya wananchi katika maeneo yetu, unakuta miradi haikamiliki na viongozi kwenye kata wapo” amesema.
Pia amesisitiza usimamizi madhubuti wa fedha za asilimia kumi (10) zinazotelewa na halmashauri kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, kwa kusema fedha hizo hazisimamiwi kikamilifu na kupelekea kuto kuwa na tija katika makundi hayo.
“Kuna kikundi kimoja cha wanawake wamepewa mkopo na kununua ng’ombe lakini mtu aliyewaletea ng’ombe hao ameleta ng’ombe hajapandishwa tena kamtoa mbali, shida mtu aliyepewa kazi hiyo hana utaalamu wowote na kuwapa mzigo kumuhudumia ng’ombe huyo” amesema.
Amebainisha kuwa ofisi yake imeandaa kitabu maalumu kinachoonyesha utekelezaji wa miradi na shughuli zote zilizofanywa na Mkoa wa Dodoma kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kikijumuisha makongamano waliyoyafanya kama Mkoa.
Pia Dkt Mahenge amewataka viongozi kwenda kuyasimamia yote waliyokubaliana kupitia kikao hicho ili wanapokutana katika vikao vingine mambo mengi yawe yametekelezeka kikamilifu ili kufikia malengo ya serikali katika kuwahudumia wananchi.
Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Maduka Kessy amewaonya wale wote wenye tabia ya kufuja mapato kwa kukusanya mapato nje ya mfumo kwa lengo la kufuja mapato hayo kwa kuwa kwa uzoefu wake mifumo hiyo ipo sahihi lakini kuna baadhi ya watu wanafanya makusudi ili zionekane hazina ufanisi katika utendaji kazi.
Nae Mbunge wa jimbo la Kibakwe Wilayani Mpwapwa ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mheshimiwa George Simbachawene ameshauri halmashauri kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa ardhi katika maeneo yao hasa baada ya ujio wa makao makuu ili wananchi wanufaike na ardhi hiyo kwa halmashauri hizo kupima ardhi kuiongezea thamani.
“Ukiangalia maeneo mengi ardhi ipo tu na watu wengi wanakuja wananunua kama mashamba hii sio sawa wananchi wetu waelimishwe umuhimu wa ardhi na ardhi hiyo ipimwe” amesema Waziri Simbachawene.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.