MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutekeleza miradi ya kimkakati inayolenga kutoa huduma kwa wananchi ikiwemo ujenzi wa soko kuu linalojulikana kama soko la Ndugai pamoja na miradi mingine ambapo amewakumbusha kuikamilisha kwa wakati.
Aliyasema hayo katika ziara yake jijini humo mapema leo asubuhi Januari 10, 2020 ambapo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi na viongozi wengine wa Mkoa huo.
Mkuu huyo wa Mkoa alipewa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo inayoendelea kujengwa katika hatua za mwisho katika Jiji la Dodoma ambayo ni ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi, soko kuu la Ndugai, uboreshaji wa bustani ya mapumziko katika eneo la Chinangali pamoja na kituo kikuu cha kuegesha malori eneo la Nala.
“Niwapongeze kwa hatua mliyofikia, mmepiga hatua katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, kwa hatua miradi hii ilipofikia nina imani tarehe mliyoahidi kuikamilisha mtakuwa tayari, Februari 15 siyo mbali hakikisheni inakuwa kama mlivyoahidi,” alisema Dkt. Mahenge.
Awali wakati wa ziara hiyo, pia Dkt. Mahenge alitembelea mtaa wa Nyakongo Kata ya Nkuhungu kukagua athari za mvua, ambapo eneo hilo limekumbwa na mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha Jijini humo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, mwenyekiti wa mtaa huo Matonya Chiwaligo alisema kuwa eneo hilo halina miundombinu ya kutiririsha maji ya mvua hali inayopelekea kuishia kwenye makazi ya watu.
Kufuatia hali hiyo, mkuu huyo wa mkoa ameziagiza mamlaka zinazohusika na miundombinu ya maji wakiwemo wakala wa barabara za mjini na vijijini (TARURA) na wakala wa barabara (TANROADS) kukutana haraka na kuweka mpango wa pamoja katika kulinusuru eneo hilo na mafuriko.
“Nawaagiza wote wanaohusika na hili, hakikisheni mnakutana mara moja ili mlipatie ufumbuzi wa haraka eneo hili, TARURA na TANROADS kupitia wataalamu wenu shirikianeni katika kulitatua hili kwa wakati kabla ya januari 30, 2020 eneo hili liwe limewekwa miundombinu ya kutiririsha maji,” alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Aidha, amewaagiza viongozi wote wa Mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanakuwa na utaratibu wa kutunza taarifa za kazi na changamoto wanazozitatua kwa wananchi na kuonyesha zilizotatuliwa na zilizopelekwa katika ngazi za juu za maamuzi ili kuboresha huduma kwa wananchi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.