MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge ametaka kufanyika kwa tathmini juu ya sera na matamko yanayohusu udhibiti wa vifo vya mama na mtoto yanayotolewa kama yanasaidia katika udhibiti wa vifo vya uzazi hapa nchini.
Dkt Mahenge ametoa ushauri huo jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha kujadili mpango mkakati wa kupunguza vifo vya mama na mtoto kinachofanyika Dodoma baina ya wakurugenzi wa Halmashauri, waganga wa hospital na wadau wa sekta ya afya kanda ya kati.
Amesema mara nyingi kumekuwa na matamko mengi na sera juu ya udhibiti wa vifo vya mama na mtoto imefika wakati kufanyatathmini kuona ufanisi wa sera na matamko hayo.
“Tuna matamko mengi na sera je zimetufikisha wapi, nashauri mkae muangalie tumefanikiwa wapi na tumekwama wapi ili turekebishe kupunguza hivi vifo vya mama na mtoto ambavyo vingi vinaepukika” amesema Dkt Mahenge.
Amesema takwimu zinaonyesha vifo vya uzazi vinaongezeka ambapo kwa mwaka 2018 hadi 2020 vimekuwa vikiongezeka licha ya mikakati iliyofanyika kwa kanda ya kati 2019 kulikuwa na vifo 162 na mwaka 2020 ilikuwa 175.
Amesema miongoni mwa vitu vinavyochangia vifo hivyo ni kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua kwa akina mama, kifafa cha mimba, kupasuka kwa mji wa uzazi na uambukizo mkali, ambavyo vinaweza kuzuilika na kupunguza vifo vya uzazi.
Ameongeza kuwa “vifo vya watoto wachanga pia ni changamoto katika kanda hii takwimu zinaonyesha kupungua kwa mwaka 2019 vifo 1,173 na mwaka 2020 kulikuwa na vifo 1,009” amesema.
Ametaja vitu vinavyosababisha vifo kwa watoto ni kushindwa kupumua baada ya kuzaliwa, mtoto kuzaliwa kabla ya wakati na mtoto kuzaliwa na uzito pungufu na neumoni.
Amewataka wakurugenzi kuhakikisha watoto wanaotakiwa kwenda shule wanakwenda ili angalau wapate elimu ambayo itasaidia kuwa na uelewa katika jamii hali itakayopunguza vifo vya uzazi kwa jamii kuwa na elimu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma ya kinga kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia wazee na watoto Dkt Leonard Subi amesema mpaka sasa wamepiga hatua kubwa katika mapambano kuzuia vifo vya mama na mtoto kwa kuimarisha huduma za Msingi na Sekondari.
Amesema katika kikao hicho watatumia katika kutathmini utekelezaji wa mpango wa mapambano dhidi ya kupunguza vifo vya uzazi hasa kwa mama na mtoto na kuweka mikakati mipya kuhakikisha wanapunguza vifo vya uzazi na kupokea utekelezaji wa mpango huo kwa halmashauri.
Amesema kwa sasa wameimarisha sana miondombinu kama hospitali, vituo vya Afya na zahanati kuhakikisha huduma hizo zinafikiwa na wananchi kwa wakati na kwa urahisi sana kupunguza vifo vya mama na mtoto ikiwa na ushirikishwaji katika ngazi mbalimbali hadi ngazi ya kaya.
Amesema kama Wizara wanafanya kila jitihada kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 vifo vya uzazi vipungue kwa kiasi kikubwa hadi kufika vifo chini ya 70 kati ya vizazi laki moja (100,000) katika kuhakikisha tatizo hilo linapungua na kuwa na takwimu sahihi amewataka wakurugenzi kupata takwimu za vifo vya uzazi kila siku asubuhi wakishirikiana na watendaji wa ngazi zote katika halmashauri zao.
“Nikiuliza hapa kila Mkurugenzi takwimu za vifo katika halmashauri yake hana jibu mpaka aulize kwa wataalamu wake kuanzia sasa nataka takwimu hizo mzipate kila siku” amesema Dkt Subi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.