MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge amewahakikishia usalama wa hali na mali zao wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza Mkoani humo huku akisema kuwa hicho ni kigezo muhimu katika shughuli za kiuchumi.
Ametoa kauli hiyo mapema mwishoni mwa wiki iliyopita ofisini kwake alipokutana na wawakilishi wa makampuni 13 ya kibiashara kutoka Austria yanayotafuta fursa za kuwekeza Jijini Mkoani humo.
Msafara wa wageni hao umeratibiwa na ubalozi wa Austria kwa kushirikiana na ubalozi wa Tanzania ambapo balozi wa Tanzania nchini Kenya Dkt. John Simbachawene aliongozana na msafara huo Mkoani Dodoma.
Mkuu wa Mkoa Mahenge aliwaeleza wageni hao kuwa, Tanzania ni nchi tulivu yenye amani na utayari wa kisiasa kupokea wawekezaji.
Alitaja baadhi ya maeneo ya msingi yenye fursa kubwa za kuwekeza kuwa ni pamoja na Viwanda, Afya, Elimu, Usafirishaji, Nishati, Ujenzi, Miundombinu na Kilimo.
Awali mchumi wa Jiji la Dodoma Shabani Juma aliwasilisha andiko linaloeleza fursa za kuweka katika Jiji hilo, ikiwemo maeneo makubwa ya ujenzi wa viwanda vikubwa na vidogo, Hoteli za hadhi mbalimbali ikiwemo nyota tano, shule za kimataifa, Hospitali kubwa, Kilimo cha Zabibu, na viwanja vya michezo.
Akizungumza kwa niaba ya msafara huo, afisa biashara kutoka ubalozi wa Austria wenye ofisi zake nchini Kenya Edith Predorf aliishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa maelezo mazuri juu ya fursa za uwekezaji zilizopo Dodoma na kuahidi kwamba makampuni hayo yataifanyia kazi taarifa hiyo na kuamua maeneo mahsusi watakayowekeza.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.