Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge ameunda Kamati maalum ya kufuatilia na kutatua kero zinazowakabili Wafanya Biashara wa Soko Kuu jipya la Job Ndugai na Kituo Kikuu cha Mabasi Dodoma na kuitaka iwasilishe kwake taarifa ya changamoto hizo ndani ya siku saba.
Mahenge ameyasema hayo kwenye mkutano na wafanya Biashara hao, uliofanyika kwenye viunga vya Soko hilo leo Nzuguni nje kidogo ya Jiji la Dodoma.
Baadhi ya changamoto zilizowasilishwa na wadau hao ni pamoja na uchache wa vizimba vya kufanyia Biashara pamoja kudhibiti mtu mmoja kumiliki vizimba vingi katika eneo la Soko na Kituo cha mabasi.
Akijibu hoja hizo Dkt. Mahenge alisema ameunda kamati itakayojumuisha, watumishi wa Halmashauri ya Jiji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, viongozi wa Soko pamoja na Kituo cha Mabasi kufuatilia changamoto hizo ili haki iweze kutendeka na kuwaahidi kuzipatia ufumbuzi ndani ya siku saba.
“Mkurugenzi na watu wake wamefanya kazi nzuri sana tuwapongeze kwa kweli, haya mengine ni changamoto ambazo tutazitafutia ufumbuzi ili tuweze kuzitatua, nimeunda timu nzuri naamini itafanya kazi nzuri na haki itatendeka” alisema Dkt. Mahenge.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Godwin Kunambi amewataka wafanya biashara hao na wakazi wa Dodoma kwa ujumla kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa mambo makubwa anayoyafanya Dodoma ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Soko kuu hilo na Kituo Kikubwa cha Mabasi.
“Mhe. Rais ameyafanya makubwa hapa Dodoma na anaendelea kuyafanya mengine, anajenga uwanja mkubwa wa ndege na miradi mikubwa zaidi inakuja, niwaombe tu kuwa makini na kuitunza miradi hiyo ili Jiji letu liendelee kuwa miongoni mwa majiji makubwa barani Afrika” amesema Kunambi.
Mhe. Binilith Mahenge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (aliyeinua mkono) akizungumza na wafanya biashara wa Soko Kuu la Job Ndugai alipotembelea soko hilo ili kuongea nao juu ya changamoto wanazokutana nazo sokoni hapo. Kushoto kwa Mhe. Mahenge ni Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi akisikiliza kwa makini.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi akifafanua jambo mbele ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Binilith Mahenge na wafanyabiashara wa Soko Kuu la Job Ndugai leo.
Mmoja wa Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Job Ndugai akielezea changamoto wanazokutana nazo sokoni hapo, ambapo katika mkutano huo na Mkuu wa Mkoa alifika ili kuwasikiliza na kuona namna bora na kuzitatua kwa maslahi ya wafanyabiashara hao na Serilkali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.