Na Binde Constantine, DODOMA.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka ametoa agizo kwa wananchi wa kaya zote za Dodoma, wanaomiliki viwanja na tayari wana umiliki wa hatimiliki ya viwanja hivyo, kuhakikisha wanapanda miti katika maeneo yao, ikiwa ni utekelezaji wa kampeni ya kimkoa ya kuhakikisha kwamba kila kaya au kiwanja kinapandwa miti.
Mtaka aliyasema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya Ismaili Civic yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari ya Bunge Septemba 26, 2021 ambapo Ismaili Civic walitoa miti 1,000 iliyopandwa katika shule hiyo, zoezi lililoongozwa na Mkuu huyo wa Mkoa.
“Sisi kama Mkoa tupo kwenye kampeni ya kuhakikisha kwamba kila kaya wanapanda miti, na changamoto kubwa ya watu wa Dodoma ni upandaji wa miti, kwa hiyo maudhui ya mwaka huu kwa mkoa wa Dodoma ni kuhakikisha wananchi wa Dodoma wanajitahidi kupanda miti” alisema Mtaka.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dkt. Fatma Mganga, alitoa wito kwa wanafunzi wa shule hiyo waitunze na kuisamamia miti hiyo ili iweze kukua na kustawi vizuri kwa lengo la kupendezesha mazingira ya shule hiyo mpya huku akiahidi kufuatilia maendeleo ya miti iliyopandwa.
“Mkuu wa shule ukishirikina na walimu pamoja na wanafunzi, naagiza muitunze miti hii iliyopandwa leo lakini na mimi nitakua nanyi bega kwa bega kutunza hii miti ili mwisho wa siku tuweze kuona matunda yake” alisema Mganga.
Aidha, Makamu wa Rais wa Jumuiya ya Ismaili Civic, Nazir Thawer alitoa wito kwa wananchi wa Dodoma kutunza mazingira ikiambatana na upandaji wa miti katika maeneo yanayowazunguka ikizingatiwa kuwa maudhui yao ya mwaka huu wa 2021 ni usimamizi na utunzaji wa mazingira.
“Katika ufanyaji wa kazi za kijamii tumejitolea wafanyakazi takribani 20,000 kidunia, wakifanya kazi kwa masaa laki moja ya kutoa huduma, mwaka huu maudhui yetu ni usimamizi na utunzaji wa mazingira, ambao utahusisha ukarabati na usafi katika maeneo ya Umma ili kuweka hali nzuri na endelevu katika maeneo yetu” alisema Nazir.
Akitoa shukrani, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bunge, Salome Elias aliishukuru ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Jumuiya ya Ismaili Civic kwa kuichagua shule hiyo kuipa msaada wa miti hiyo kwani itasaidia katika kutengeneza mazingira rafiki ya kujisomea kwa wanafunzi wake na aliahidi kutunza miti hiyo.
“Sisi kwetu ni baraka kwa sababu tuna changamoto ya upepo kwahiyo tukiona watu wanatusaidia tunaona dalili za mabadiliko, nitumie fursa hii kuahidi watu wote mliopo hapa leo na kwako Mkuu wa Mkoa kwamba hii miti tutaitunza” alisema Mkuu huyo wa shule.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.