MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka ameitaka Taasisi ya Teknolojia Dar es saalam (DIT) kupitia kampuni yake tanzu kusajili bunifu zake ili kuzilinda dhidi ya watu ambao wamekuwa na tabia ya kuiba bunifu.
Mtaka ameyasema hayo leo Juni 14,2022 jijini Dodoma wakati wa Maonyesho ya bunifu mbalimbali zilizofanywa na taasisi hiyo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma. Mtaka, amesema kuwa kumekuwepo na watu ambao wamekuwa wazuri katika kuiba bunifu za watu wengine hivyo kama taasisi hiyo haitakuwa makini inaweza kujikuta katika wakati mgumu.
“Niwapaongeze kwa bunifu mnazofanya lakini mnapaswa kuzisajili na kuanza kuzifanyia kazi au kuziuza kwani hizo bunifu ni fedha, hamna sababu ya kuendelea kulalamika wakati mmekaa na bunifu kama hizi kwenye makabati” amesema Mtaka.
Mtaka ameichagua taasisi hiyo kufanya kazi kwa wafanyakazi wa bodaboda kwa kutembelea baadhi ya wilaya zilizopo Mkoani humo. Amesema DIT inauwezo mkubwa katika ufanyaji wa kazi zake na imezalisha wabunifu wengi katika bunifu mbalimbali.
“Mnauwezo mkubwa na ndio maana leo tumewachagua kufanya kazi na Dodoma ambapo kesho mtaanza kuwasajili wanaofanya kazi ya bodaboda, Ubunifu huu umekuwa wa kipekee sana na tunataka tuone mkiendelea kubuni bunifu mbalimbali ambazo nchi nyingine zitaiga kutoka kwetu” amesema Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma.
Hata hivyo, amewashauri wakuu wa wilaya za Dodoma kuitumia taasisi hiyo ili kupata mifumo mbalimbali itayo wasaidia kujibu kero mbalimbali katika maeneo yao.
Meneja Masoko wa kampuni ya DIT, Agnes Kimwaga, amesema kuwa Taasisi hiyo imeanza kubiasharailisha bunifu mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na wanafunzi wake ili kwenda kujibu changamoto zilizopo katika jamii. “Kampuni hii itaweza kuuza bunifu zote ambazo zimefanywa kwa kuzipeleka sokoni na kuziuza badala ya kubaki katika makabati bila kuwa na tija” amesema Kimwaga.
Aidha, amesema kuwa kabla ya kuanzishwa kampuni hiyo tanzu bunifu nyingi zilikuwa zinabaki na kufungiwa kwenye makabati ofisini bila kuwa na manufaa kwa taasisi na jamii. “Tumekuwa tukiandaa bunifu mbalimbali kupitia wanafunzi wetu lakini zinaishia kwenye makabati sasa tumeamua kuzibiasharailisha bunifu zote ili kwenda kujibu changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii” amefafanua Kimwaga.
Hata hivyo Kimwaga amemshukuru Mtaka kwa kuwa tayari kufanya kazi pamoja na DIT. “Tunamshukuru sana Mhe. Mtaka kwa kuwa tayari kufanya kazi pamoja na sisi na kesho tunaanza na hiyo ya bodaboda ambayo imetengenezwa na Dkt. Budoya.
“Na kikubwa zaidi tumekaribishwa kila wilaya na sisi tutaenda kila wilaya ambazo tumekaribishwa na tutafika pia mpaka ngazi ya kata na tutakuwa tumefanya kazi kubwa”. Amemalizia Kimwaga.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.