MKUU wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka amelitaka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kuandaa mkutano wa tathimini ya maonyesho ya vyuo vya ufundi ili kuona tija ya maonyesho hayo.
Kauli hiyo aliitoa jana mara baada ya kutembelea mabanda ya Taasisi mbalimbali katika maonyesho ya pili ya elimu ya mafunzo na ufundi yaliyoandaliwa na NACTE kwa kushirikiana na Taasisi ya sekta binafsi (TPSF) yanayoendelea katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Mtaka amesema kuwa watafanya kikao cha kujadili namna pia ya kuwaendeleza wabunifu wa maonyesho hayo ili kazi zao ziwe na tija kiuchumi zaidi.
“Naomba NACTE baada ya maonyesho haya kuhitimishwa,muandae mkutano wa tathimini tukae pamoja na tujadili mambo mablimbali ya maonyesho haya zikiwemo changamoto ili tujue namna ya kuzitatua ili tukapoandaa maonyesho ya mwakani yawe na tija zaidi.”amesema Mtaka
Pia ameitaka NACTE kuhakikishe mwakani mkoa unakuwa ni sehemu ya maandalizi ya mashindano haya,ili kusaidia kutangaza maonyesho hayo kikamilifu na kutoa hamasa kwa wananchi kuja kutembelea mabanda na kununua bidhaa zinazouzwa.
Mtaka amesema kuwa lengo la kufanya hivyo ni pamoja na kutaka kuboresha maonyesho hayo ya vyuo yaliyoandaliwa na NACTE ili yawe na msisimko zaidi kwa wananchi.
“Naamini kwamba maonyesho yajayo yakiboreshwa yatabadili taswira na kuwa sehemu ya kuchevusha biashara ya mkoa ikiwemo kukuza teknolojia katika sekta mbalimbali kama Kilimo,ufugaji na vingine.” amesisitiza.
Pia Mhe.Mtaka amesema kuwa wao kama Mkoa wako tayari kushirikiana na waandaaji wa maonyesho ikiwemo kuwa na sehemu ambayo italea na kukuza wabunifu ambao watakuwa wamebuni teknolojia mbalimbali kupitia kwenye maonyesho husika.
Aidha Mhe.Mtaka amewaomba waandishi wa habari kuhakikisha wanashirikiana na NACTE au taasisi nyingine zote kuhakikisha wanayatangaza maonyesho hayo kwa siku zilizobaki ili jamii ijue na kujitokeza kutembelea katika viwanja hivyo.
Hata hivyo amezishauri Benki na Taasisi za fedha kutenga fedha kwa ajili ya kuwadhamini wabunifu nchini ili kuendeleza vipaji vyao.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa NACTE Dkt.Adolf Rutayuga amesema kuwa wao kama NACTE watayafanyia kazi ushauri na maoni yote aliyoyatoa ili kuleta tija zaidi katika maonyesho hayo mwakani.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.