Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka, amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu Mzee John Samweli Malecela ambapo ametumia nafasi hiyo kumshirikisha Mzee Malecela vipaumbele vyake katika Mkoa wa Dodoma na kupokea ushauri wa kiongozi na mwanasiasa huyo Mkongwe hapa nchini.
Mhe. Mtaka aliyemtembelea Mzee Malecela nyumbani kwake eneo la uzunguni hapa Jijini Dodoma, amemwelezea Mzee Malecela kuwa kipaumbele chake cha kwanza hapa Mkoani Dodoma ni Elimu na kazi iliyombele ni kunyanyua kiwango cha Elimu na Ufaulu katika Mkoa wa Dodoma. Katika kuleta mabadiliko hayo ya Elimu, Mhe. Mtaka amesema atashirikiana na viongozi wazawa wa Mkoa wa Dodoma, wadau wote wenye jukumu la kusimamia elimu kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya na Mamlaka za Serikali za Mitaa hadi Ngazi za Msingi hali kadhalika sekta binafsi.
Akitaja kipaumbele kingine Mhe. Mtaka amesema atageukia sekta ya kilimo kwa kuzifanya Wilaya za Pembezoni za Mkoa wa Dodoma (Wilaya zinazozunguka Wilaya ya Dodoma) kuwa Kanda Maalum za Kilimo na kukifanya Kilimo cha Mkoa wa Dodoma kuwa cha kibiashara huku mkazo akiuweka kwenye zao la Zabibu kama alama ya Mkoa wa Dodoma, Alizeti na mazao mengine ya kuzalisha mafuta ya chakula. Amesema kilimo kitasaidia kukuza uchumi wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma na Mkoa kwa ujumla.
Mhe. Mtaka amemwelezea Mzee Malecela kuwa mahitaji makubwa ya mafuta ya chakula yanayoilazimu nchi yetu kuagiza mafuta nje ya nchi, ni fursa kubwa ya kiuchumi kwa Mkoa wa Dodoma ambao mazao yanayotumika kuzalisha mafuta kama Alizeti, Karanga na Ufuta yanastawi vizuri katika Mkoa wa Dodoma.
Katika Mazingira, Mhe. Mtaka amesema ataendesha kampeni ya Mkoa ya Upandaji na ustawishaji miti katika Mkoa Mzima wa Dodoma itakayo shirikisha Wadau wa ngazi mbalimbali kuanzia Mkoa, Wilaya, Tarafa, Kata, Vijiji, Vitongoji na ngazi za kaya. Mhe. Mtaka amemtaja Mzee Malecela kama mfano wa kuigwa wa wana mazingira ambao walifanikisha kupanda miti mingi kwenye maeneo waliyokuwa wanayaongoza.
Nae Mzee Malecela ameshukuru kwa mazungumzo yaliyowezesha kubadilishana uzoefu na Mkuu wa Mkoa Mtaka, amesema Dodoma ina fursa kubwa ya kilimo cha mazao yanayokamuliwa kuzalisha mafuta ya chakula huku akizitaja Wilaya za Kongwa na Mpwapwa kama maeneo yenye hali ya hewa nzuri kwa uzalishaji wa Karanga tangu miaka ya zamani, ametaja maeneo ya Wilaya zingine za Dodoma yanafaa sana kwa kilimo cha Alizeti na Zabibu.
Amemtaka Mkuu wa Mkoa Mtaka kuweka mkazo pia kwenye sekta ya ufugaji kwa kutambua Mkoa wa Dodoma una idadi kubwa ya mifugo ambayo ni fursa nyingine ya kukuza uchumi wa Mkoa huku akibainisha kuwa pamoja na Mkoa kubahatika kuwa na kituo kikubwa cha utafiti wa mifugo cha Mpwapwa na shamba kubwa la Mifugo la Serikali lililopo Kongwa bado rasilimali hizo hazijasaidia kubadilisha jamii za Wafugaji wa Mkoa wa Dodoma kuweza kuwa na tija katika ufugaji wao huku wakiendelea kufuga mifugo kienyeji.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.