MKUU wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amekutana na kufanya mazungumzo na Wafanyabiashara wakubwa Mkoani Dodoma kwa lengo la kupokea maoni yao kuhusu Mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji katika Mkoa wa Dodoma.
Kikao hicho kilichofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, kimewajumuisha Wafanyabiashara wakubwa kutoka sekta mbalimbali, wakuu wa Taasisi zinazotoa huduma na zinazosimamia masuala ya biashara na uwekezaji zikiwemo Idara ya Kazi, Wakala wa Vipimo, TANESCO, TARURA, DUWASA, TIC, TRA, TBS, OSHA, TMDA na Viongozi wa Halmashauri ya jiji la Dodoma.
Mtaka amewaeleza wafanyabiashara kuwa yeye ni muumini Mkubwa wa Sekta Binafsi kwa kutambua ukweli kuwa ndio wachavushaji wa uchumi kukua na kwamba licha ya Serikali kuwa Muajiri Mkuu, Sekta Binafsi imeendelea kuwa muajiri wa wakati wote huku ikiwa na fursa lukuki za kufanya uchumi na uzalishaji.
“Tukitaka jiji la Dodoma liwe shindani ndani na nje ya jumuiya ya Afrika Mashariki, liweze kushindana na majiji kama Nairobi, Kampala, Bujumbura, Kigali na Majiji mengine makubwa nje ya Afrika, lazima Sekta Binafsi ijipambanue na kustawisha shughuli zake na katika kipindi cha uongozi wangu kama Mkuu wa Mkoa wa Dodoma nitahakikisha Serikali inailinda Sekta Binafsi” alibainisha Mhe. Mtaka.
Aliwataka Wadau wa Sekta Binafsi katika Mkoa wa Dodoma kujipanga vema ili kuweza kufaidika na fursa za kuwekeza zinazotokana na Serikali kuhamishia shughuli zake Makao Makuu ya Nchi na hata wanapokuja Wawekezaji wakubwa kutoka Nje ya Nchi, Sekta Binafsi waweze kuingia nao mashirikiano katika uwekezaji mbalimbali.
Nae Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Wakulima na Wenye Viwanda Mkoa wa Dodoma – TCCIA Ndg. Deus Nyabiri ameitaka serikali kupitia Mamlaka ya Mapato TRA kuhakikisha inaongeza program za utoaji elimu ya kodi na kuhakikisha inawafikia Wafanyabiashara wote kuanzia Wakubwa hadi wajasiriamali wadogo ili wawe na utamaduni wa kulipa kodi wao wenmyewe bila kushurutishwa.
Aidha, ameitaka Halmashauri ya Jiji la Dodoma kushindana na majiji mengine makubwa ndani na nje ya Afrika kwa kuboresha miundombinu ya maeneo ya kufanyia biashara kama vile masoko, vituo vya mabasi na kuweka mifumo rafiki ya uendeshaji ambayo haitageuka kero kwa wananchi wanaotegemea huduma hizo.
Ametoa Rai kwa Uongozi wa Mkoa wa Dodoma kuhakikisha inahuisha mabaraza ya biashara ya Mkoa na Wilaya na Majukwaa ya Kodi ili yafanye kazi yake ya msingi ya kuwa majukwaa ya majadiliano kati ya wafanyabiashara/wawekezaji na serikali na taasisi zake ili kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji katika Mkoa wa Dodoma.
Kwa upande wake Mjumbe wa TCCIA Taifa Ndg. Faustine Mwakalinga amezitaka Taasisi mbalimbali za Serikali zinazosimamia shughuli za biashara na uwekezaji kufanya kazi kwa ushirikiano kama timu mmoja ili kuondoa urasimu, usumbufu na ucheleweshaji wa utekelezaji miradi kwa kuchelewesha au kukwamisha vibali mbalimbali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.