Na Nemes Michael, DODOMA.
“TUTAWAHESHIMU, tutawapenda na kuwatetea, nataka mfanye kazi kwa kujivunia pia kujiamini, sekta binafsi ni kipaumbele katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma sababu ndio uchumi na maendeleo katika Mkoa huu”.
Hiyo ni kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka katika mkutano na wadau wa sekta binafsi uliofanyika ofisini kwake ukiwa na lengo la kutatua changamoto za biashara kwenye sekta hiyo ili kuwawezesha kuongeza wigo wa biashara na kuchangia maendeleo ya Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Mtaka amesema kuwa, ni wakati sahihi kukutana na wadau wa sekta binafsi na wajasiriamali kwani wamekuwa na uchochezi katika maendeleo mkoani hapa, sanjari na hayo amewataka wajasiriamali hao kuheshimiana licha ya kwamba kuna utofauti wa kipato na kuhimiza kuwasiliana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakati wowote wanapokumbana na changamoto.
"Dodoma tuna maeneo makubwa ambayo tayari yameshatengwa kwa ajili ya uwekezaji yakiwa na miundombinu ya umeme na maji, ni nafasi na fursa ambazo kwa pamoja tunatakiwa kuzikimbilia ili kuleta maendeleo katika mkoa wa wetu na uchumi binafsi" amesema Mtaka.
Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza kuwa, katika kuleta taswira sahihi ya Mkoa wa Dodoma ambao ni Makao Makuu ya Tanzania tuna wajibu wa kushirikiana ili kuweza kuleta ushindani wa kiuchumi na miji mingine mikuu ya Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, mjasiriamali kutoka kampuni inayojihusisha na ardhi ya ‘Land Network Ltd’ Samwel Ikwabe alisema kuwa, uamuzi wa Mkuu wa Mkoa kukutana na wajasiriamali ni sahihi na wenye faida kwa pande zote mbili katika maendeleo ya Mkoa wa Dodoma na Taifa kwa ujumla.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.