MKUU wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka, ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa yanayojengwa kupitia fedha za mapambano dhidi ya UVIKO- 19 ambapo Mkoa huo unatarajia kukabidhi madarasa 601 Disemba 30 mwaka huu.
Hayo ameyasema leo Disemba 22, 2021 jijini Dodoma mara baada ya kufanya ziara pamoja na Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Dodoma ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari.
Mtaka amesema kuwa ujenzi wa madarasa unakwenda vizuri na matarajio ya mkoa ni kukabidhi vyumba vyote vya madarasa ifikapo Disemba 30 mwaka huu. “Kama mkoa tumeridhika na hatua ya ujenzi ilipofikia na tunataraji kufanya hafla ya kukabidi vyumba hivi 601 vya mkoa katika wilaya mojawapo ambayo tutaichagua kwa niaba ya mkoa” amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Aidha Mtaka ameziagiza wilaya zote ambazo zinatekeleza mradi huo wa ujenzi wa vyumba vya madarasa kuhakikisha kuwa zinapanda miti katika maeneo ya shule. “Wakati madarasa haya yanajengwa naomba yaendane na zoezi la upandaji wa miti, haiwezakani shule inakuwa na majengo mazuri lakini maeneo yake yamepauka lazima kila mwanafunzi apate mti mmoja wa kuutunza” amesema Mtaka.
Hata hivyo Mtaka amewataka wazazi na walezi ambao watoto wao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kuhakikisha ifikapo Januari 17 Mwaka 2022 watoto wote wawepo shuleni. “Itakuwa ni aibu kubwa kuwa na majengo mazuri na ya kisasa ambayo yanajitosheleza lakini watoto hawaendi shule, hatutaki kuona watoto wanaonekana sokoni, mitaani pamoja na mashambani au kuwa sehemu ya kutunza familia” amesisitiza Mtaka.
Pia ameutaka uongozi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha unakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa wakati ili watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza waweze kusoma.
Kwa upande wake Katibu Tawala mkoa wa Dodoma Dk. Fatma Mganga, amesema kuwa ujenzi wa vyumba vya madarasa 601 unagharimu kiasi cha Sh. bilioni 12.02 kwa shule za sekondari, lakini pia mkoa wa Dodoma unajenga madarasa 175 kwa ajili ya shule shikizi ambayo yataghalimu kiasi cha Sh.bilioni 3.5.
Awali Mkurugenzi wa jiji la Dodoma Joseph Mafuru ameihakikishia Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Dodoma kuwa hadi ifikapo Disemba 24 mwaka huu madarasa hayo yatakuwa tayari. “Sisi kama Jiji tunajitahidi katika kutekeleza mradi huu na tunamshukuru sana mheshimiwa Rais kuona umuhimu wa watoto ambao walikuwa wanakosa nafasi kuweza kusoma" alisema Mafuru.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka akimuangalia mmoja wa mafundi wa 'tiles' akiendelea na kazi wakazi wa ziara yake ya ukaguzi wa maendeleo ya kazi za ujenzi wa madarasa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mkata akikagua ujenzi wa madarasa akiwa ameambatana pia na maafisa kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru akiongea kuhusu utekelezaji wa shughuli za ujenzi wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.