Na Nemes Michael, DODOMA.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amewataka Wakuu wa Wilaya walio teuliwa kutumia nafasi zao kwa hekima na siyo mabavu.
Aliyasema hayo katika viwanja vya ofisi ya Mkoa kwenye halfa fupi ya uapisho wa Wakuu wa Wilaya wapya leo tarehe 22 Juni 2021.
Mtaka aliongeza kuwa nafasi waliyonayo ni kumwakilisha Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungamo wa Tanzania na siyo Mkuu wa Mkoa, hivyo wajikite kwenye kuhakikisha wanatatua changamoto za wananchi katika maeneo yao.
“Mimi nina wasaidizi wangu lakini siyo ninyi, kila mmoja abebe thamani kwamba amepewa heshima ya kumsaidia Rais kwenye wilaya aliyoteuliwa, nawasisitiza kuwa uongozi ni utumishi na utumishi ni hekima ukitawala kinguvu utaharibu ila hekima hujenga” aliongeza Mtaka.
Kwa upande wake, Mkuu Wilaya ya Kondoa Khamis Mkanachi alisema kuwa nafasi aliyopewa kuhudumu katika Wilaya hiyo ni deni ambalo atalilipa kwa utumishi uliyotukuka na kuhakikisha anatoa mchango chanya kwa maendeleo ya Mkoa wa Dodoma na nchi kwa ujumla.
“Mkuu wa Mkoa nimekufuatilia katika vipaumbele ulivyoahidi tangu siku ya kwanza unakabidhiwa ofisi ambavyo ni Kilimo cha kisasa, Elimu, Afya, Maji, Uwekezaji, Sekta binafsi na Haki kwa watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla naambatana na wewe katika kusimamia vipaumbele hivyo” aliongeza Mkanachi.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Remedius Emmanuel amemshukuru Rais Samia kwa kumteua na kumuamini kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo na kusema kuwa anaahidi ushirikiano kwa mkuu wa mkoa na wananchi katika maendeleo na utatuzi wa changamoto.
Mkuu huyo wa wilaya ameongeza kuwa kazi yake kubwa ni kuhakikisha anatimiza maono, matarajio, na mategemeo ya Rais Samia kuyatekeleza katika wilaya ya Kongwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.