Na Noelina Kimolo, DODOMA.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka amewataka Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo kutambua kuwa wao ni wawakilishi wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Wilaya zao hivyo wafanye kazi huku wakitambua dhamana waliyoibeba.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa hafla fupi ya uapisho wa Wakuu wa Wilaya wapya wa Kongwa na Kondoa iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa mapema leo Juni 22, 2021.
Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka Wakuu hao wa Wilaya wawe na ushirikiano wa kutosha na viongozi mbalimbali katika wilaya, ili kuendeleza kasi ya maendeleo makubwa kwenye mkoa huo ambao ni Makao Makuu ya Nchi.
“Tengeneza hadidhi yako kwa kuleta maendeleo katika sehemu ambayo unakuwepo, hata ukiondoka watu waone kitu ambacho umekifanya” alisema Mtaka.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Khamis Mkanachi, alisema kutokana na imani ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwake, atahakikisha kuwa anafanya kazi kwa juhudi kwa kushirikiana na viongozi wenzake pamoja na wananchi wa Wilaya ya Kondoa kwa ujumla.
“Kuanzisha kilimo cha kisasa, elimu, afya na sekta binafsi ni vitu ambavyo wewe Mkuu wa Mkoa uliahidi kuvipa kipaumbele, tunaambatana na wewe kwa hayo uliyoyaonesha kama dira na sisi tutayasimamia haya kwa kiwango cha juu” alisema Mkanachi.
Aidha, alisema kuwa wao ni watumishi na siyo watawala, wanakwenda kuhudumia jamii na wanatamani kuonesha utofauti kwa huduma watakayotoa katika jamiii ili imani walizopewa zikaonekane.
Naye mkuu wa Wilaya ya Kongwa Remedius Emmanuel, alisema anahitaji sana ushirikiano kutoka kwa Wakuu wa Wilaya wengine, viongozi pamoja na wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku.
“Kazi yangu ni kutekeleza ile imani ambayo Mhe. Rais ameionesha kwangu kama kijana, na hivi karibuni alisema atachagua vijana, sasa mimi ni miongoni mwa hao vijana hivyo kazi yangu ni kuendelea kuleta mchango wa vijana katika Taifa letu” alisema Emmanuel.
Wakuu hao wa Wilaya waliteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi karibuni ambapo kwa mujibu wa taratibu wataapishwa na Wakuu wa Mikoa husika.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.