Na. Josephina Kayugwa, DODOMA.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ametoa agizo kwa wataalamu wanaosimamia miradi mbalimbali katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuangalia namna gani ambavyo sehemu ambazo hazijatumika muda mrefu kutokana na sababu mbalimbali zinaanza kufanya kazi mapema ili zianze kuongeza mapato kwa Halmashauri pamoja na mwananchi anayetumia eneo hilo.
Agizo hilo alilitoa katika majumuisho ya ziara aliyoifanya ya kutembelea miradi mbalimbali ikiwemo Stendi ya Mabasi Nanenane, Soko kuu la Job Ndugai pamoja na Dodoma City Hotel, miradi inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kuongeza mapato ya ndani.
"Nia ya kujenga miradi hiyo siyo ikae wazi bila kutumika hatimaye kuharibika bali kuongeza kipato kwa mtumiaji na Jiji hivyo wataalamu inatakiwa mkae muangalie na mbuni mbinu mpya za jinsi gani sehemu hizi zitaanza kufanya kazi mapema.
Mfano hapa soko la Job Ndugai kuna sehemu nyingi hazifanyi kazi ila wapangaji wamelipia hii ni hasara kwao na kwetu kwa sababu haikuwa lengo la mradi hivyo inaweza kubuniwa namna nyingine ya kupatumia kama maonesho, minada hata kwa wiki mara moja ili kuchangamsha mradi na kuutangaza sehemu mbalimbali kupitia hayo maonesho ya ndani na nje," alisema Senyamule.
Aidha Mkuu wa Mkoa alisema wananchi wanatakiwa kufundishwa kutumia vitu vyao vilivyojengwa na Serikali kwa kutumia kodi na kuifanya Dodoma kuwa fahari ya watanzania kweli kwa sababu ya kutimiza malengo ya miradi hii.
Alisema wataalamu washirikiane na wataalamu wengine katika kutangaza maeneo haya kwa wananchi ili wapate kuyajua vizuri kwa sababu lengo ni kuongeza mapato na sehemu hizi zitumike vyema na kutoa huduma mbalimbali.
Sambamba na maagizo aliyoyatoa hakusita kuipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutekeleza miradi mikubwa na yenye ufanisi wa hali ya juu, miradi itakayoongeza mapato kwa Serikali na wananchi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.