MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kwa kutekeleza agizo la Serikali la kuhakikisha Taasisi zinaanzisha, kusimamia na kutekeleza dhana ya michezo kwa Viongozi na watumishi.
Senyamule ametoa pongezi hizo wakati akizindua Bonanza la Siku ya Michezo ya Mamlaka hiyo, lenye lengo la kuhamasisha wafanyakazi kushiriki michezo na kufanya mazoezi ili kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
“Naipongeza DUWASA kwa kutekeleza Agizo la Serikali la kuhakikisha Taasisi zinaanzisha, kusimamia na kutekeleza dhana ya michezo kwa Viongozi na watumishi wake na hata ikitokea wengine wakaanza mfano utabaki kuwa wa kwenu DUWASA kwa sababu mmekuwa wa kwanza kabisa kuanzisha michezo hii na itawasaidia kujenga afya na utimamu wa mwili.
Na kuongeza kuwa “kupitia Bonanza hili la DUWASA natoa maagizo kwa Taasisi zote za umma mkoa wa Dodoma kutekeleza maagizo ya serikali kwa watumishi wake kushiriki mazoezi na michezo kwa ajili ya kulinda afya na kujiandaa kushiriki Mashindano ya SHIMUTA ya mwaka huu,” amesema Senyamula
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya DUWASA amewaasa watumishi kubadili mienendo ya maisha inayohatarisha afya zao hali inayoweza kudhoofisha ufanisi wa kazi.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph amezungumzia , malengo ya kufanyika kwa Bonanza la Siku ya Michezo, amesema ni utekelezaji wa maagizo ya serikali pamoja na DUWASA kuhakikisha watumishi wanakuwa na afya njema wakati wa kutekeleza majukumu yao na itawasaidia kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari na shinikizo la damu.
Katika Bonanza hilo watumishi wa DUWASA wameshiriki michezo mbalimbali, ikiwemo mbio fupi, mpira wa Pete na miguu, kufukuza kuku, riadha na mbio za magunia ambapo washindi wamezawadiwa vikombe vya ushindi na fedha taslimu.
Uzinduzi wa Bonanza la Siku ya Michezo DUWASA limefungua mwendelezo kwa watumishi wote kushiriki mazoezi kila Ijumaa ya kila wiki baada ya muda wa kazi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.