MKUU wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amewataka Wakuu wa Shule za Mkoa huo kuanzia ngazi ya Elimu msingi na Sekondari kuhakikisha wanatoa ripoti ya utoro na maendeleo ya wanafunzi kila ifikapo Ijumaa ya kila wiki kuanzia ngazi ya kata mpaka mkoa ili kudhibiti utoro kwa wanafunzi.
Hayo ameyasema wakati akifungua kikao kazi cha kukabidhi mkakati wa kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji ngazi ya elimu msingi na sekondari kwa Maafisa elimu,Wakuu wa Shule za Mkoa wa Dodoma pamoja na wadau wa elimu jumatano katikati ya wiki hii ya Septemba tarehe 07,2022.
Aidha Senyamule amewataka maafisa elimu na wakuu hao wa shule kuwa wabunifu katika kutatua changamoto mbalimbali zinazozikabili shule za mkoa wa Dodoma na wao kutokuwa chanzo cha changamoto hizo.
"Msiwe sehemu ya matatizo kazi kubwa mliyopewa ni kutatua matatizo hasa nyie maafisa elimu ambapo Mkuu wa shule anakuletea changamoto badala ya kutatua wewe unakuwa sehemu ya hiyo changamoto niwaombe tatueni changamoto pindi zinapowafikia," Amesema Senyamule.
Pia Mhe. Senyamule amewataka Maafisa Elimu kutokaa Ofisini muda wote wakati kuna shule nyingi za kutembelea na kubaini changamoto zilizopo na kuzitatua na sio kutumia muda mwingi kuandika taarifa wakiwa ofisini.
Kwa upande wake Katibu tawala wa Mkoa wa Dodoma Dkt.Fatuma Mganga amesema kuwa ameona ipo haja ya kubadili gia katika sekta ya elimu kutokana na matokeo ya Moku Mkoa wa Dodoma kutoridhisha.
"Bila kuchukua maamuzi magumu katika sekta hii nyeti ya elimu tutaendelea kuona viwango vyetu kama mkoa zinazidi kushuka siku hadi siku ni vyema tukachukua hatua za haraka kiukweli hatupo nafasi nzuri kabisa na mjue tu sisi ni jicho kila mmoja anatuangalia sisi tu, " Amesema Mganga.
Nae Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru amesema kuwa hawatakuwa tayari kuendelea kukaa na watendaji ambao hawatekelezi majukumu yao vizuri kuendana na kasi inayohitajika hivyo watapeleka mapendekezo kwenye ofisi ya katibu tawala ili kwa wale ambao wameonakana hawatendi kazi kisawasawa kwani ndio wanaosababisha tuendelee kuwa nyuma.
"Siku sio nyingi tutaanza kuwaondoa watendaji ambao wanatukwamisha kufikia malengo yetu nitahakikisha naleta majina ya watendaji wa ngazi yeyote ile wanaotukwamisha maana kuna watumishi wanatamani sana kufanya kazi hapa ila waliopo hapa wanaendelea kuchezea nafasi hizo ukweli tutaondoana ili kila mmoja alinde nafasi yake" Amesema Mafuru.
Kikao kazi hicho cha wadau wa elimu mkoa wa Dodoma kimekaliwa ili kuleta mawazo yatakayosaidia kuleta mageuzi ya elimu itakayoendana na hadhi ya makao makuu nchi.
DODOMA FAHARI YA WATANZANIA
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.