RC Senyamule akabidhiwa cheti cha shukran na SHIVYAWATA, Dodoma
Imewekwa tarehe: December 29th, 2024
Na. Hellen M. Minja,
Habari – DODOMA RS
UONGOZI wa Muungano wa Vyama vya Watu Wenye Ulemavu SHIVYAWATA wamefika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma iliyopo katika jengo la Mkapa Jijini Dodoma kwa lengo la kumshukuru Mkuu wa Mkoa Mhe. Rosemary Senyamule kwa kufanikisha hafla ya chakula cha pamoja wakati wa maadhimisho ya siku ya walemavu Duniani yaliyofanyika Disemba 6, 2024.
Shukrani hizo zimekwenda sanjari na kumkabidhi cheti cha shukrani kwa kutambua mchango wake wa hali na mali katika kufanikisha Kongamano la siku mbili kuelekea maadhimisho hayo lililofanyika Disemba 5 na 6 katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Waliofika ofisini hapo kwa niaba ya uongozi ni Bw. Jastus Ngwantalima na Bw. Enock Mbana.
Kauli mbiu iliyoongoza Maadhimisho ya mwaka huu ilikua “Kukuza Uongozi wa Watu Wenye Ulemavu kwa Ajili ya Mustakabali Jumuishi na Endelevu"