MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amemtembelea Mkulima maarufu ambaye ni mjane Bi. Melisia Samwel Mbalamwezi nyumbani kwake Mtaa wa Mayeto, Kata ya Hombolo Makulu, Jijini Dodoma kwa lengo la kujionea ubunifu alioufanya kwenye sekta ya kilimo cha ndizi katika eneo lake la ukubwa wa takribani heka 40.
Ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kukagua miradi na kusikiliza na kutatua kero za wananchi Mhe. Senyamule amefanikiwa kutatua changamoto ya Barabara kuelekea shambani kwa Bi. Melisia.
Aidha, ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji kuhakikisha anatengeneza miundombinu ya Barabara wezeshi hadi kufika katika eneo hilo, pamoja na kumtafutia soko la bidhaa zake na kupatiwa elimu juu ya kilimo cha kisasa kutoka kwa watalaam ili kukifanya kuwa na tija .
Sanjari na hilo, Mkuu huyo wa Mkoa ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia za kubweteka na kujifunza kupitia mkulima huyo.
"Watu wengi wakishakuwa wajane huwa wanajinyong'onyesha lakini nikupongeze Bi. Melisia, tunayo mambo mengi ya kujifunza kutoka kwako, kwa sababu umekuwa mwananchi wa mfano kwa kuonesha utayari wa kutekeleza ajenda ya Tanzania kuwa ghala la chakula. Hivyo, Serikali ina mambo mengi ya kukusaidia kwa sababu tayari umesha jiandaa" ameelekeza Mhe. Senyamule.
Kwa Upande Wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Bw. John Kayombo ameahidi ushirikiano wa karibu na haraka kwa mkulima huyo kwa kupatiwa kipaumbele kwa changamoto mbalimbali ambazo atakuwa nazo kwa hoja ambazo zinahitaji watalaam, masoko na mikopo inayotolewa na Serikali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.