WANANCHI wa Mtaa wa Vyeyula Kata ya Mkutupola, Jiji la Dodoma wametakiwa kutokuwa na hofu kuhusu mpaka wa Bonde la Mzakwe wakati Serikali ikiendelea kufanya takwimu na uchunguzi wa kina kuhusu suala hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Mtaa Vyeyula na kusema kuwa, zipo sababu mbalimbali zilizopelekea eneo hilo kutokuwa na utatuzi. Mojawapo ya sababu ni kutofahamu idadi halisi ya wananchi wanaoishi katika eneo hilo, kutofahamu mipaka halisi iliyopitiwa na kiasi cha maji katika Bonde hilo.
"Sababu zinazopekekea kutofanya maamuzi sahihi ni kwasababu kwanza haijulikani kama kweli maji hayo bado yapo, idadi ya watu waliopitiwa na Bonde hilo na sababu nyingine nyingi hivyo, niwatoe hofu wananchi wa Kata ya Vyeyula kwasababu tunatuma timu ya wataalam kuja kuchunguza kwa undani suala hilo” alisema Senyamule.
Aliongeza kwa kusema kuwa kuanzia tarehe 14 mpaka 21 februari, 2024 kutakua na wataalam watakaofanya kazi ya kukagua na kuchukua takwimu za usahihi kuhusu maeneo hayo yaliyopitiwa na Bonde la Mzakwe.
"Kuanzia kesho timu ya wataalam kutoka ofisi ya Takwimu watakuja kuchunguza suala hilo ili kupata majibu sahihi. Hivyo, niwaombe mtoe ushirikiano wa kutosha ili tupate ufumbuzi wa suala hili lakini pia muendelee kuwa na amani na utulivu wakati Serikali ikiendelea kufanya kazi yake na msiwe na wasiwasi" aliongezea.
Kwa upande wake mtaalam kutoka ofisi ya Takwimu Afisa Mfumo ya Kijiografia, Jerrve Gasto alisema taarifa mbalimbali zinahitajika katika takwimu hizo ili kujua ni aina gani ya watu wanaoishi katika eneo hilo thamani ya majengo na shughuli za kiuchumi wanazojihusisha nazo.
"Tutaongea na wakuu wa kaya ili kupata taarifa zao kamili juu ya mazingira wanayoishi, thamani ya majengo na shughuli za kiuchumi wanazojihusisha nazo. Niwaombe wananchi mtoe ushirikiano ili tumalize kazi hii mapema zaidi" alisema Gasto.
Kwa upande wake, Mrisho Shabani mkazi wa mtaa wa Vyeyula aliiomba serikali ifanye hima kumaliza jambo hilo kwani imekua ni tatizo la muda mrefu. "Tunaomba serikali ifanye hima kumaliza jambo hilo kwani imekua ni tatizo la muda na mrefu sana. Ni kero kwetu sote pia tunaomba wataalam hao watoe elimu sahihi ili kuwe na wepeii zaidi kwa kutekeleza jambo hili kwa haraka zaidi" alisema Shabani.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.