Redio za ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma zimekuwa na mchango mkubwa katika kuwafundisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Elimu Sekondari wa Halmashari ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha 'Dodoma Live' kinachorushwa na kituo cha redio Dodoma FM kupitia masafa ya 98.4 leo asubuhi.
Mwalimu Rweyemamu amesema kuwa katika kipindi cha mapumziko ya mapambano ya dhidi ya virusi vya corona baada ya shule kufungwa wanafunzi walikuwa wakizurura mitaani kwa kukosa kazi ya kufanya.
"Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliona kuwa hilo ni tatizo kwa ukuaji wa sekta ya elimu na mapambano dhidi ya virusi vya corona. Halmashauri ikaamua kuja na mkakati wa kunusuru sekta hiyo kwa kubuni mpango wa kuwafundisha wanafunzi kupitia vipindi vya redio zilizopo ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma na mitandao ya kijami kama youtube. Katika kufanikisha dhamira hii, redio zimekuwa na mchango mkubwa sana. Nawapongeze redio Dodoma FM kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kukuza sekta ya elimu jijini Dodoma" alisema Mwalimu Rweyemamu.
Akijibu swali juu ya walengwa wa progamu hiyo, amesema kuwa imelenga wanafunzi wa kidato cha pili na kidato cha nne na wanafunzi wa darasa la nne na la saba ambayo ni madarasa ya mitihani.
Katika kuhakikisha elimu hiyo inawafikia na kuwanufaisha wananfuzi wengi, Afisa Elimu huyo amewataka wazazi kusikiliza redio Dodoma FM na redio za ndani ya jiji la Dodoma na kuwahimiza wanafunzi kusikiliza redio hizo ili kunufaika na vipindi vinavyoendelea na kufanya mazoezi kadiri yanavyotolewa na walimu wabobezi. Kuhusu ratiba amesema kuwa inapatikana katika tovuti a Jiji la Dodoma www.dodomacc.go.tz na kwa watendaji wa kata na mitaa, walimu na wakuu wa shule zote jijini Dodoma.
Ikumbukwe kuwa mkakati wa kuwanusuru wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wa jiji la Dodoma ulizunduliwa na Mkurungenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi tarehe 28 Aprili, 2020 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashari ya Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.