RAIS Mteule wa Kenya, Dkt. William Ruto leo tarehe 13 Septemba, 2022 ameapishwa kuwa Rais wa tano wa nchi hiyo baada ya Rais Uhuru Kenyatta kumaliza muda wake wa kutawala taifa hilo la Afrika Mashariki.
Sherehe za kumuapisha Ruto zimefanyika kwenye Uwanja wa Kasarani jijini Nairobi na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi, pamoja na viongozi wa nchi mbalimbali akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.
Akihutubia viongozi mbalimbali pamoja na wananchi wa Kenya katika sherehe za uapisho wa Rais Dkt. William Samoei Ruto, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewapongeza wakenya kwa kuonesha ukakamavu wa demokrasia na kumaliza uchaguzi salama.
Rais Samia katika moja ya nukuu zake amesema "Ndugu zangu wakenya kama kuna zawadi mliyoitoa kwa wana jumuiya ya Afrika Mashariki basi ni zawadi ya amani katika uchaguzi wenu, hongereni sana.
Nitumie fursa hii kuihakikishia Kenya dhamira yetu ya dhati ya kufanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu zaidi katika kuleta maendeleo ya pamoja ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi zetu na pia ukanda wote wa Afrika Mashariki." Amesema Rais Samia.
Akimalizia hotuba yake fupi, Rais Samia amewaasa wakenya kwa kusema "Ndugu zangu wakenya, sasa uchaguzi umeisha hivyo muungane kama wakenya kuhakikisha mnaijenga nchi kwa pamoja bila kuwepo utofauti wa aina yeyote." Alimalizia Rais huyo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pichani juu anaonekana Rais Samia wa Tanzania (kushoto) akimpongeza Rais William Ruto (kulia) baada ya kula kiapo cha kuiongoza nchi ya Kenya.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.