WAKALA wa Maji na Usafiri wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Dodoma umedhamiria kufikisha maji Vijijini kwa asilimia 85 kama inavyosema ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hayo yamebainishwa leo Mei 31, 2024 kwenye kikao cha Watumishi wake wote wa Mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.
Kikao hicho kilichokwenda sambamba na mafunzo kwa Watumishi juu ya namna ya kujiandaa kustaafu Mapema, kimehudhuriwa na Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ambaye amewasihi kutimiza azma hiyo.
"Takwimu zinaonesha, kabla ya kuanzishwa RUWASA, maji yalifika Vijijini Mkoa wa Dodoma kwa asilimia 57.4 lakini tangu kuanzishwa kwake, umepanda hadi kufikia 66.3%. Niwapongeze sana. Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inataka kufikia 2025, muwe mumefikia 85%. Kutokana na mikakati muliyojiwekea, nina imani mutaweza kufikia lengo". Amesema Mhe. Senyamule
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Kaspar K. Mmuya, ambaye alikuwepo kwenye kikao hicho, amesema kuwa Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa mikoa inayokua kwa kasi hivyo ifikapo June 2025, maji yapatikane kwa zaidi ya asilimia 85. Aidha, amewataka kushughulikia changamoto za upatikanaji maji na kutojihusisha na rushwa.
Akizungumzia mafanikio ya Taasisi yake, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Dodoma Injinia Ally Mbaraka, amesema mpaka Sasa vijiji 416 vya Mkoa wa Dodoma vimefikiwa na huduma ya maji ambapo ni zaidi ya 50%. Serikali imetoa shilingi Bilioni 6 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Maji na kwa mwaka mpya wa fedha (2024/25) wanatarajia kupokea shilingi Bilioni 19.
RUWASA ilianza kutekeleza majukumu yake kama Taasisi mnamo Tarehe Mosi July, 2019 kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za maji maeneo ya Vijijini. Mpaka Sasa imefanikiwa kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo kupitia kauli mbiu ya "RUWASA, Maji bombani" na mpaka sasa Mkoa wa Dodoma unatekeleza miradi 75 ya maji kwenye Halmashauri zote za Dodoma itakayowezesha kufikia lengo la 85% ifikapo 2025.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.