TAASISI ya Mashauriano ya Kisheria ya Nchi za Asia na Afrika (AALCO), imetakiwa kusimama kidete katika kulinda maslahi ya nchi zinazoendelea, kwa kuweka utaratibu mzuri na sheria za kimataifa dhidi ya mataifa yanayochochea migogoro katika nchi hizo, kwa maslahi yao binafsi.
Pia, taasisi hiyo imeombwa kuonesha mchango wake na kupaza sauti katika jitihada za kuyashawishi mataifa yaliyoiwekea vikwazo vya kiuchumi nchi ya Zimbabwe, kuondoa vikwazo hivyo.
Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam jana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati akifungua Mkutano wa 58 wa AALCO uliokutanisha washiriki zaidi ya 150 kutoka mataifa mbalimbali wanachama wa taasisi hiyo.
“Leo hii tunashuhudia vita ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi mbalimbali zinazoendelea zilizosababishwa na mataifa yenye ubinafsi kwa lengo la kujichukulia rasilimali katika nchi hizo zenye migogoro,” alieleza Samia.
Alisema ni wakati wa taasisi hiyo kusimama kidete na kuweka taratibu nzuri na sheria za kimataifa zitakazodhibiti mataifa hayo yenye ubinafsi. Pamoja na hayo, aliiomba taasisi hiyo kupitia mkutano huo kusaidia kuhamasisha mataifa yaliyowekea vikwazo nchi ya Zimbabwe kuviondoa kwa kuwa kwa sasa nchi hiyo ni taifa huru linalojitegemea.
“Serikali ya Tanzania tunaamini kuwa wanachama wa AALCO kupitia mkutano huu watatumia sauti zao kuhakikisha wanaendeleza kanuni ya kutoingilia mambo ya ndani na heshima kwa uhuru wa dola husika,” alieleza.
Chanzo:HabariLeo Online
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.