WAWEKEZAJI wa ndani na nje wametakiwa kujipanga kuwekeza katika Halmashauri ya jiji la Dodoma kutokana na fursa nyingi zilizopo baada ya jiji kuwa makao makuu ya nchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alipoongoza timu ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi walioshiriki kongamano la uwekezaji lililofanyika jijini hapa kwa siku mbili kutembelea fursa za uwekezaji katika mji wa serikali jana.
Kunambi alisema kuwa kutokana na uamuzi wa Rais Dkt John Magufuli kuhamishia serikali katika Halmashauri ya jiji la Dodoma, uamuzi huo umefungua fursa nyingi za uwekezaji. “Sisi Halmashauri ya jiji la Dodoma, tunamshukuru sana Rais, Mheshimiwa Dkt John Magufuli, uamuzi wake wa kihistoria kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi umefungua fursa nyingi za uwekezaji na biashara katika jiji hili. Hivyo, natoa wito kwa wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza katika jiji la Dodoma. Tunataka muwekezaji mwenye fedha akija anapewa eneo anaanza ujenzi, hatutaki kuchelewa” alisema Kunambi.
Vilevile, aliwataka watumishi wa umma kufanya uamuzi wa kujenga nyumba za makazi katika jiji hilo mapema. “Nitoe rai kwa watumishi wenzangu wa umma, baada ya serikali kuhamia Dodoma, watumishi wengi wamehamia Dodoma. Chukueni viwanja muanze kujenga makazi sasa. Kama hujajenga Dodoma, njoo ujenge sasa. Dodoma ndiyo habari ya mjini” alisisitiza Kunambi.
Akiongelea umuhimu wa utunzaji wa mazingira, Mkurugenzi huyo alisema kuwa, ongezeko la watu linaenda sambamba na ongezeko la joto kutokana na changamoto ya uharibifu wa mazingira. Halmashauri ya Jiji imejipanga katika kuhamasisha upandaji miti katika maeneo yote ili jiji lipate sehemu ya kupumulia, aliongeza. “Kila eneo tunalopima na kutenga eneo la wazi, wananchi wenyewe watapanda miti na kuihudumia ili kulifanya jiji letu kuwa rafiki kwa mazingira bora.
Kongamano la Uwekezaji la Mkoa wa Dodoma limefanyika kwa siku mbili katika Halmashauri ya jiji la Dodoma likihudhuriwa na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi waliopata fursa ya kujadili fursa za uwekezaji na kutembelea maeneo mbalimbali yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji na miradi mikubwa ya uwekezaji.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.