Na. Mussa Richard, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepanga kujenga viwanja vya michezo ikiwemo uwanja wa mpira wa miguu uliopo katika mchakato wa ujenzi, kuelekea michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 ambapo kwa pamoja nchi za Afrika Mashariki Tanzania, Kenya na Uganda zitakuwa wenyeji wa michuano hiyo.
Mpango huo umewekwa wazi na Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Francis Kaunda kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Dkt. Frederick Sagamiko, wakati akiwasilisha Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 katika Baraza Maalum la Madiwani, lililofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kwa upande wake Daudi Fundikira, Diwani wa Kata ya Chang'ombe baada ya kupitishwa kwa Bajeti hiyo alisema "Tumepanga kujenga viwanja vya michezo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambavyo vitakua ni sehemu ya kuongeza mapato kwa jiji letu la Dodoma, lakini pia ni fursa kwa vijana wetu kufanya mazoezi na kuweza kuonekana, kwani michezo ni ajira na michezo ni burudani”
Aidha, Diwani wa Kata ya Chamwino, Jumanne Ngede, alielezea faida za ujenzi wa viwanja hivyo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kwa jamii kiujumla. "Kwanza nimpongeze sana Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Dkt. Frederick Sagamiko na timu yake kwa mpango huu mzuri wa ujenzi wa viwanja, kwasababu faida zake si kwa Halmashauri tu kuingiza kipato, bali hata kwa wananchi, mfano wafanyabiashara wadogo wataweza kufanya biashara zao na kupata wateja zaidi kutokana na muingiliano wa watu utakao kuwa unafanyika viwanjani". Alisema Ngede.
Kwa mujibu wa wasilisho la Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Francis Kaunda alisema Mpango wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni shilingi 147,910,202,949.46, ikipanga kukusanya mapato ya ndani kiasi cha shilingi 67,385,000,000.00, ruzuku za mishahara ikiwa ni shilingi 65,739,308,000.00 ruzuku ya matumizi mengine ikiwa ni shilingi 3,071,349,000,00 na ruzuku ya miradi ya maendeleo ikiwa ni shilingi 11,714,545,949.46. Bajeti hiyo ikiongezeka kwa asilimia 7.04 kulinganisha na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.